📌Ni kufuatia upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Njiro
📌Kituo chafungwa transforma yenye MVA 210 kutoka MVA 90 ya awali
📌Dk. Biteko aipongeza TANESCO kuendelea kuwapa watanzania huduma ya umeme wa uhakika
Arusha
MKOA wa Arusha sasa umewezeshwa kupata umeme wa uhakika baada ya upanuzi wa Kituo cha kupooza na kusafirisha umeme cha Njiro, kwa kuongeza Transfoma yenye uwezo wa MVA 210 kutoka MVA 90 ya hapo awali.

Akizungumza na wananchi katika hafla za Sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkoani Arusha, mara baada ya kuzindua kituo hicho Aprili 26 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo hicho ili kukiongezea Kituo uwezo kuendana na ongezeko la matumizi ya umeme.
“Katika ukanda huu, mahitaji ya umeme kwenye Mkoa wa Arusha ni megawati 107, Tanga Megawati 126, Manyara Megawati 14, na Kilimanjaro Megawati 68, na leo tumezindua upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Njiro, ambacho kina njia kumi za kusambaza umeme katika Mkoa wa Arusha na kuuwezesha Mkoa huu kukidhi mahitaji ya umeme kufikia Megawati 200 kulinganisha na mahitaji ya sasa ambayo ni Megawati 107,” amesema Dk. Biteko.
Aidha amesema kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa utekelezaji wa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ikiwa ni maagizo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha miundombinu ya umeme chakavu yote inafanyiwa ukarabati wa njia za kusafirisha umeme.

“Umeme tunaweza kuwa nao kwenye uzalishaji, lakini ikawa changamoto kwenye miundombinu, ndio maana Mhe. Rais ametuagiza sasa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ili tuwe na umeme wa uhakika,” amesema Dk. Biteko.
Ameongeza kwa kusema kuwa Wizara ya Nishati imekusudia kuhakikisha kila Mtanzania anapata kipande cha keki ya Nishati hasa Nishati ya umeme.
“Nilipoteuliwa niliwaambia, TANESCO hamtalala usingizi, na wote mnashuhudia kuwa hali ya umeme imebadilika sio kama miaka kumi nyuma, na TANESCO kwa kweli hawalali wanafanya kazi nzuri” amsema.

Kukamilika kwa Kituo hicho kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Mkoa wa Arusha na kuifungua kiuchumi kwa kukuza Sekta za Utalii, Viwanda na Biashara.