Home KITAIFA RAIS DK.SAMIA ANATARAJIA KUWA MGENI RASMI ‘Samia Kalamu Awards’

RAIS DK.SAMIA ANATARAJIA KUWA MGENI RASMI ‘Samia Kalamu Awards’

Dar es Salaam

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji tuzo za waandishi wa habari zinazofahamika kama “Samia Kalamu Awards” itakayofanyika Aprili 29, 2025 jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 15, 2025 jijini Dar es Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk. Rose Reuben amesema tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni tuzo maalum za kutambua  mchango wao katika kuandika habari za maendeleo.

Amesema kuwa tuzo hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza  kwa lengo la kuhamasisha na kuthamini kazi za waandishi wanaojikita katika uandishi unaoleta uelewa, hamasa na mabadiliko chanya katika jamii.

 Ameeleza kuwa Samia Kalamu Awards ni matokeo ya mafunzo yaliyotolewa kwa wanahabari mwaka 2024, kwa lengo la kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.

 “Tunataka kuona habari zinazoibua changamoto lakini pia zikitafuta suluhisho. Hii ni njia mojawapo ya kuonyesha kuwa uandishi wa habari una nafasi muhimu katika maendeleo ya taifa letu,” amesema Dk. Reuben.

Amebainisha kwamba tuzo hizo zimegawanywa katika makundi makuu matatu. Kundi la kwanza linahusisha tuzo za umahiri wa kitaifa pamoja na tuzo maalum kwa waandishi wanawake, maafisa habari wa serikali na wachapishaji wa mitandaoni. 

Kundi la pili linajumuisha vyombo vya habari kama redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii. Kundi la tatu ni tuzo za kisekta zinazohusu maeneo kama afya, maji, elimu, kilimo, mazingira, TEHAMA, uchumi wa buluu, vijana, sanaa, michezo, utalii, na uwekezaji.

Amewataka waandishi wote nchini kushiriki kikamilifu katika tukio hilo, wakisisitiza kuwa ni jukwaa muhimu la kutangaza mchango wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Ameweka wazi kuwa hafla hiyo itarushwa mubashara kupitia vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii, ili kuwapa wananchi nafasi ya kushuhudia mchango wa wanahabari waliobobea katika kuelimisha na kuleta mabadiliko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here