Home KITAIFA MAWAKILI WASISITIZWA KUISHAURI SERIKALI KWA WELEDI

MAWAKILI WASISITIZWA KUISHAURI SERIKALI KWA WELEDI

đź“ŚDk. Biteko asema Serikali inatambua jitihada za Asasi za Kiraia kuhudumia Wananchi

đź“ŚRais Samia apongezwa kwa mageuzi katika huduma za sheria nchini

đź“ŚWawakili wahimizwa kuwa ‘marafiki’wa Mungu badala ya Mahakama

đź“ŚDkt. Biteko ataja mikakati ya Serikali kuboresha huduma za sheria kwa wananchi

Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na kuhakikisha haki inatendeka miongoni mwa wanajamii.

Dk. Biteko amesema hayo leo Aprili 15, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini.

“Ombi langu kwenu Mawakili wa Serikali, fanyeni kazi yenu kwa kuzingatia taaluma yenu ya sheria na kutenda haki, ni wajibu wenu kushauri kwa haki na fanyeni kazi bila kuathiriwa na maslahi ya mnaowashauri wala kuogopa,” amesema Dk. Biteko.

Amesisitiza kwa kuwataka mawakili kufanya kazi ya kuiwezesha Serikali kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia misingi ya haki.

“Fanyeni kazi ya kutetea Serikali yenu, nendeni mkaishauri Serikali na wakati wote mkatende haki, ifanyeni haki kuwa rafiki yenu na anayetokea mbele yenu aone haki imetendeka hata watakaokuwa wamehukumiwa wakiri wanastahili hukumu waliyopewa,”amesema.

Dk. Biteko amewapongeza Mawakili wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa kuunda na kuendesha Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za Ushauri wa Kisheria bila malipo katika mikoa mitatu ya Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.

Amesema kuwa Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Asasi za Kiraia, na binafsi katika kuwahudumia wananchi kupata huduma za sheria huku akitaja baadhi ya asasi na vyama hivyo kuwa ni pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) pamoja na Watoa Huduma za Msaada wa kisheria kama UNDP na UN Women.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amemuelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokikabili Chama hicho cha Mawakili wa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata eneo la kujenga Ofisi za Makuu ya Chama na Vivutio vya Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika mikoa ya Arusha na Dodoma

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni. Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Rais Dk. Samia ameimarisha sekta ya sheria kwa kutekeleza masuala mbalimbali mfano kusaidia uwepo wa haki jinai na Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia.

Amesema kuwa umuhimu wa mkutano huo wa Mawakili wa Serikali kuwa ni kuwapa fursa kukutana na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, maslahi yao pamoja na kufahamiana.

Amewapongeza waasisi wa Chama hicho kwa kujenga taswira nzuri huku akiwaasa viongozi wengine watakao fuata kuendeleza taswira hiyo na amewataka mawakili hao kuwa marafiki wa Mungu badala ya Mahakama kwa kutenda haki na kusema kweli wakati wa kutimiza majukumu yao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwa mkezi wa chama hicho kwa miaka mitatu na kusema kuwa ni wajibu wao sasa kukilinda na kuhakikisha kinafikia malengo yaliyokusudiwa.

Pia, amebainisha kuwa kupitia mkutano huo wameidhinisha Mpango Mkakati wa Chama hicho kitakachoufuata na kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano.

“Tumetengeneza Mpango Mkakati tunaokwenda kuutekeleza kwa shauku kubwa pamoja na viongozi wapya watakao chaguliwa katika Uchaguzi unaofanyika leo,” amesema Johari.

Amesema hadi kufikia Aprili 9, 2025 idadi ya mawakili wa Serikali imefikia 3,760 kutoka 2,652 waliosajiliwa wakati wa kuanzishwa kwa Chama hicho.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Dk. Mwinyi Talib Haji amewaomba Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria ili kujenga jamii imara na kupunguza mizozo katika jamii.

Amesema taasisi za sheria ziendelee kushirikiana ili kusaidia wananchi na kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuhudumia jamii na kuleta ustawi kwa mustakabali kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Amedeus Shayo amesema Chama kimefanikiwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa kukusanya ada kwa wanachama pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoshughilika na masuala ya sheria za ndani na nje ya nchi.

“ Rais Samia ameendelea kuwa kielelezo kizuri cha haki kupitia Kampeni yake ya Msaada wa Kisheria na Mawakili wanashiriki kutoa huduma za sheria kwa wananchi. Pia, agizo la Rais Samia la Mawakili kuwa walinzi wa uchumi wa nchi kwa kutumia kalamu limeweka msingi wa Chama hiki na umesaidia kuboresha sheria kadhaa mfano Sheria ya Uwekezaji,” amesema Shayo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu na Jaji wa Mahakama Kuu, Dk. Eliezer Feleshi amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuzindua Chama hicho mwaka 2022 na kusema “ Chama hiki kama kilivyoanzishwa na malengo yake kitabaki kuwa Chama bora cha kitaaluma kwa sababu Serikali na mawakili walijipanga kuwa nacho na hili ni jeshi la kulinda uchumi wa nchi kwa sheria na kalamu,”

Mkutano huo uliohudhuriwa na Mawakili wa Serikali kutoka katika Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali, Mashirika ya umma umeongozwa na Kauli mbiu “ Utawala wa Sheria katika Utekelezaji wa Majukumu ya Serikaki ni Nguzo Muhimu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here