Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Lembrus Mchome amemuomba Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini kubatilisha maamuzi ya Baraza Kuu la Chadema lililofanyika Januari 22 mwaka huu.

Wakati suala la waraka ulioandikwa na baadhi ya wanachama wa Chadema maarufu kama g55 ukiendelea kufukuta Mchome ambaye pia ni miongoni mwa wafuasi wa G55 pia alimtaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema Tundu Lissu kukubali kukosolewa na wanachama ili kuweza kujenga chama katika kushika dola.
Akizungumza leo Aprili, 8 2025 na waandishi wa habari Mchome amesema kikao cha Baraza Kuu ambalo pia kilimthibitisha Katibu Mkuu, John Mnyika pamoja na viongozi wengine wakuu saba si halali kwakuwa akidi ya wajumbe wa kikako hicho haikuwa imetimia kama inavyoelekezwa katika katiba ya chama.
Amesema kiutaratibu ili kikao kianze ni lazima mwenyekiti awe na orodha lakini katika kikao kile katibu mkuu anakiri ni kweli hawana akidi kwakuwa hawakuwa na orodha na kama alikuwa nayo basi aipeleke kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili aihakiki.
“Katika kikao cha Baraza Kuu Mnyika alieleza kwamba kwakutazama kwamba kuna wajumbe ambao akidi haijatimia lakini hapo hapo wakaanza kikao tangu lini katibu ukaruhusu kikao kianze wakati idadi ya watu hawajatimia,unatuambuaje hawa watu waliopo wamefika asilimia 50 kama huna paper (katarasi) mezani kwako yenye orodha ya wajumbe wa baraza kuu zikiwemo sahii zao,”amesema Mchome.
Amesema mambo hayo kuyatakia ufafanuzi kama mwanachama si usaliti ila yana lengo la kujenga ili waweze kuyarekebisha.
Amesema pia amemuomba Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha maamuzi yote yaliyofanywa Januari 22 kwakuwa hayakuwa na uhalali kulingana na aina ya wajumbe waliyoyapitisha.
Pia amemuomba Msajili wa Vyama amtake Katibu Mkuu wa Chadema aitishe Baraza kuu lenye akidi ya asilimi 75 ili viongozi waliopitishwa awali wapatikane kwa usahihi.
“Naamini msajili atayafanyia kazi nimesoma barua yake naamini chama changu kitapeleka majibu kabla ya tarehe kumi,chama chetu ni chama chakidemokrasia lazima tuonyeshe mfano wa demokrasia kama tunavyowahubiria,” amesema.
Mchome ametaja hoja yake nyingine ni kuwalalamikia watu walioruhusiwa kupiga kura katika kikao hicho si wajumbe wa baraza kuu na walipiga kura.
“Katiba yetu ya chama ya mwaka 2009 kwenye kanuni za uendeshaji wa chama ya 7:3:2 inasema patakuwa kupigwa kura na wanaopaswa kuwepo pale ni wajjumbe halali tu wa kikao lakini baraza kuu linakwenda kupiga kura la kumdhibitisha katibu mkuu huku kuna watu wapo ndani si wajumbe wa baraza kuu,”amesema Mchome.
Amesema kupitia video mbalimbali za mkutano huo kuna watu walionekanawanapiga kura kumpitisha naibu Katibu Mkuu Zanzibar lakini si wajumbe wa Baraza Kuu la chama.
“Tunasema haya ili kuweka sawa chama chetu wengine walikuwa wagombea ukumbini kulikuwa na watu zaidi ya 80 ambao si wajumbe wa Baraza Kuu.Nafanya haya kwa mapenzi mema ya chama changu ,kukilinda na kukisaidia chama changu kesho na keshokutwa,”amesema Mchome.
Amesema hoja zake zake alizotoa mbili zina mashiko na zipo kwa ajili yakikusaidia chama chake kwakuwa wamekuwa waumini wakuwasindikiza watu wafuate katiba ya vyama vyao na ya nchi.
“Uchaguzi mkuu wa ndani ya chama ulioanza tarehe 20 mpaka 22 ulikuwa wakidemokrasia lakini viongozi wetu wanaonekana sio waumini wa demokrasia,”amesema .