▪️Aridhishwa na kasi na ubora wa ukarabati
Zanzibar
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi wa kuridhia Mashindano ya AFCON na CHAN kufanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza na kukuza sekta ya michezo na utalii nchini.

Akizungumza baada kukagua ukarabati na ujenzi wa Viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar leo Aprili 7, 2025, Majaliwa amesema Watanzania watapata fursa ya kuendeleza michezo na kuhamasisha wachezaji kufanya mazoezi zaidi ili wapate sifa za kucheza michuano hiyo.
“Ujio wa wageni wakati wa michuano utahitaji malazi, chakula na usafiri hivyo waliowekeza kwenye hoteli na vyombo vya usafiri watapata faida kubwa na kujiingizia kipato, hii ni fursa nzuri ambayo Marais wetu Dk. Samia na Dk. Mwinyi wametuletea kwa sababu timu zinakuja na watu wengi,”amesema.
Aidha Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na bora wa ukarabati wa viwanja hivyo unaofanywa na kampuni za REFORM na ORKUN “Kampuni hizi zimetujengea viwanja vilivyo na ubora unaokubalika”

Ameongeza kuwa jukumu lililopo kwa sasa ni kuilinda miundombinu hiyo ili ubora uliofikiwa baada ya ukarabati uendelee kuwepo hadi michuano hiyo itakapofanyika.
“Watanzania wanatamani kuvitumia viwanja hivi lakini wanatakiwa wajue kwamba viwanja hivyo kwa sasa viko kwenye ukaguzi maalum unaofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika hivyo ni muhimu kuweka utarabu ambao hautaathiri ubora ulipo,”amesema.
Pia amesema kuwa pale inapobidi serikali hawatazuia viwanja hivyo kutumika katika michezo mikubwa ila kinachotakiwa ni kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara baada ya matumizi ili kulinda ubora wake utakaoiwezesha nchi kukidhi vigezo vya kuendesha mashindano hayo .

Waziri Mkuu amesema mashindano hayo yataleta manufaa makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii na biashara.
“Hii ni fursa nzuri ambayo Marais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi wametuletea kwa sababu timu zinakuja na watu wengi,”amesema.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ni miongoni mwa viongozi waliombatana na Waziri Mkuu katika ukaguzi wa viwanja hivyo.