Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi kuiishi falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha mahusiano na kukuza diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Majaliwa amesema kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, kilimo, biashara pamoja na kupata masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Ameyasema hayo leo Aprili 6, 2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Balozi Hamad Khamis Hamad Balozi wa Tanzania nchini Msumbuji na Balozi Holmes Matinyi, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa Jijini Dodoma.

Majaliwa amesema Serikali ina mategemeo makubwa na mabalozi hao, hivyo wanapaswa kwenda kuendeleza mahusiano mazuri ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na mataifa hayo.
Waziri Mkuu amesema pamoja na mambo mengine mabalozi hao wanatakiwa wahakikishe wanasimamia vizuri matumizi ya fedha katika ofisi zao pamoja na kuanzisha au kuendeleza madarasa ya kufundisha lugha ya kiswahili.