Ruvuma
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa msingi wa sera za CCM utabakia kuwa ni maendeleo ya watu pamoja na amani na utulivu wa nchi.

Balozi Nchimbi aliyasema hayo leo Jumapili, leo Aprili, 6 2025, alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Songea katika maeneo ya Liziboni, Uwanja wa Majimaji na Mshangano, ambapo wananchi walikusanyika kwa hamasa kubwa kumsikiliza licha ya kuwa kwenye ziara nyingine za kikazi.
Katika eneo la Liziboni, Balozi Nchimbi amelazimika kusimamisha msafara wake ili kuzungumza na wananchi waliomsimamisha njiani akitokea Nyasa.

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Songea kwa mchango wao mkubwa uliomuwezesha kufahamika kitaifa na kimataifa.
Katika Uwanja wa Majimaji, amehutubia umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakimsubiri wakati alipofika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa lenye fremu 50 za CCM Mkoa wa Ruvuma. Katika hotuba yake, amewaomba wananchi wa Songea, mkoa mzima na nchi nzima kwa ujumla kujiandaa kushiriki kwa wingi Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.

Akiwa Mshangano, ambako alizindua rasmi fremu 50 za tawi la CCM la eneo hilo, Dk.Nchimbi amesisitiza tena umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi mkuu, akieleza kuwa ni kwa njia hiyo ndipo maendeleo na ustawi wa taifa yanaweza kufikiwa kwa kasi na kwa manufaa ya wote.

Kwa ujumla, ziara ya Katibu Mkuu huyo ilionesha mapokezi makubwa ya wananchi na kiu ya kusikia mwelekeo wa chama chao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.