
Wizara ya Afya imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya mkazi wa Daraja mbili mkoani Arusha Bi. Neema Kilugala aliyejifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha, Mount Meru mnamo Machi 24, 2025.
Taarifa ya leo Aprili, 2 2025 iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya, Roida Andusamile imeeleza kuwa Neema anadai kuwa baada ya kujifungua alioneshwa mtoto wake na muuguzi akiwa ni mzima.
Hata hivyo aligundua kuwa amebadilishiwa mtoto wake baada ya kuletewa mtoto akiwa amefungwa na vitenge ambavyo si vya kwake. Muuguzi wa hosptali hiyo alidai kuwa alichanganya vitenge na vya mtoto mwingine hivyo akaahidi kwenda kubadilisha, pamoja na kuchukua hatua hiyo bado kulikuwa na hali ya sintofahamu.
Kufuatia hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha pamoja na Jeshi la Polisi imechukua hatua ya kuchukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Sambamba na hilo Wizara ya Afya imechukua hatua ya kumsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia Neema ili kupisha uchunguzi kabla ya kuchukua hatua stahiki na kutoa taarifa rasmi baada ya uchunguzi kukamilika.