Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itahakikisha kuwepo kwa utii wa viongozi katika utendaji wa taasisi za umma Ili kuepusha mifarakano baina ya watendaji.

Rais Dk. Mwinyi ameeleza hayo alipozungumza katika Kongamano la Pili la Kiimani kwa Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililofanyika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni, Wilaya ya Mjini.
Amefafanua kuwa kukosekana kwa utii wa viongozi kumekuwa ndio chanzo cha fitna, majungu na mifarakano baina ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma.
Ameeleza kuwa amekuwa akipokea taarifa nyingi za kuwepo kwa ugomvi katika taasisi za umma baina ya watendaji wenye dhamana Jambo ambalo Serikali inadhamiria kuliondosha.

Akizungumzia suala la utoaji wa zaka amesema kuwa ni suluhisho la umasikini miongoni mwa jamii pale zaka inapotolewa kwa usahihi na kuwafikia watu wenye uhitaji.
Amesema endapo zaka itatolewa kwa usahihi na kuifuata miongozo ya sheria za kiislamu kundi kubwa la Watu wangetoka katika dimbwi la umasikini.

Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali kwa kupitia Afisi ya Mufti Mkuu itaendelea kusimamia yaasisi Ili suala la ugawaji wa zaka lifanyike kwa usahihi zaidi.
Akizungumzia Kuhusu amani amesema ndio suala muhimu zaidi katika nchi na kila mmoja kwa nafasi aliyonayo anapaswa kuhubiri amani.

“Kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa hapa Zanzibar kunalenga kudumishwa kwa amani na kuwanasihi wanasiasa kushirikiana na Serikali kufanikisha azma hii kwa manufaa ya nchi,” amesema.
Amesisitiza kuwa nchi haipaswi kurudi nyuma katika mifarakano ya kisiasa kwani kunachangia kuporomoka kwa uchumi na kushindwa kuleta maendeleo.
Pia ameishukuru afisi ya Mufti Mkuu kwa kusimamia vizuri na kuendeleza mambo yote ya dini ya Kiislamu ikiwemo kongamano hilo la kiimani kwa viongozi wa Serikali.