Home KITAIFA DK. SAMIA: VIONGOZI WA DINI HIMIZENI AMANI YA NCHI NA KULEA WANANCHI...

DK. SAMIA: VIONGOZI WA DINI HIMIZENI AMANI YA NCHI NA KULEA WANANCHI KIROHO

Dar es Salaam

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kuendelea kudumisha amani ya nchi na kubaki kwenye jukumu la kuwalea wananchi kiroho.

Rais Dk. Samia ameyasema hayo leo Machi, 31 2025 katika Baraza la Eid El-Fitr lililofanyika kitaifa Mkoa wa Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Amewasisitiza viongozi wa dini zote nchini kutoruhusu majukwaa ya kiimani kutumika kuhubiri siasa, au ajenda za kisiasa kuvuruga amani ya nchi kupitia majukwaa ya ibada. 

“Muwadhibiti wachache walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki dhidi ya Serikali yao. Ni vyema tujue katika mifarakano na hasama hakuna atakeyeibuka mshindi. Jukumu la kusimamia amani ni la Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama lakini pia ni jukumu la wananchi wote,” amesema Rais Dk. Samia.

Pia Dk. Samia ameweka wazi kuwa kamwe Serikali haitamvumilia yeyote atakayechochea chuki na uhasama na kusababisha uvunjifu wa amani, bali Serikali imejidhatiti kulinda haki na utu wa kila Mtanzania. 

Kwa upande mwingine, amewasihi waislamu kuwa wanaposherehekea Eid El-Fitr waendeleze ucha Mungu waliouonesha katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzilinda ibada zao na kudumisha umoja na mshikamano waliokuwa nao kipindi cha mfungo.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dk. Samia amewasisitiza wadau wote wa kisiasa kutimiza wajibu wao na kutokuruhusu itikadi za kisiasa kuwagawa Watanzania. 

Ameeleza kuwa milango ya Serikali iko wazi kusikiliza madai ya wadau wa kisiasa kupitia majukwaa mbalimbali ambayo yanawapa nafasi ya kuzungumza na majukwaa ambayo yaliwezesha mageuzi mbalimbali kufanyika kwa kuwashirikisha wadau wote wa kisiasa, ikiwemo kufutwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa na kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here