Home KITAIFA MOI YAANDIKA HISTORIA KWA KUANZA KUFANYA UPASUAJI WA UBONGO KWA KUTUMIA AKILI...

MOI YAANDIKA HISTORIA KWA KUANZA KUFANYA UPASUAJI WA UBONGO KWA KUTUMIA AKILI UNDE.

Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza rasmi upasuaji wa ubongo kwa kutumia teknolojia ya akili unde ‘Brain Lab- Neuro Navigation System’ ambayo husaidia wataalam kufanya upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo kwa ufanisi mkubwa (high efficiency & accuracy) kupitia tundu dogo hivyo kupunguza muda wa upasuaji na wa mgonjwa kukaa wodini baada ya upasuaji huo.

Hayo yamebainishwa leo Machi 27, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Taasisi hiyo.

Dk. Mpoki amesema Taasisi ya MOI ndiyo hospitali ya kwanza Tanzania kufanya upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde.

“Kwa mara ya kwanza katika nchi yetu (Tanzania) leo tumefanikiwa kufanya upasuaji wa ubongo kwa kutumia kifaa maalum ( Brain Lab- Neuronavigation System) ambacho kinamuongoza daktari kuanzia kupanga upasuaji kabla ya kufungua fuvu, wakati wa upasuaji wenyewe kwa tundu dogo kwenye fuvu na kuwezasha kumuongoza mpasuaji iwapo uvimbe umeisha wote kabisa. Teknolojia hii ambayo haitumii mionzi ya X- Ray” ni salama kabisa kwa wataalam na mgonjwa anayepata matibabu,” amesema Dk. Mpoki.

Aidha, ameongeza kuwa upasuaji huo umeongozwa na daktari bingwa mbobezi mzawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell New York cha nchini Marekani na kutoa wito kwa Watanzania wenye matatizo ya uvimbe au watakaogundulika kuwa uvimbe kwenye ubongo kufika katika Taasisi hiyo kupatiwa matibabu.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, Dk. Laurent Mchome amesema kwamba ushirikiano kati ya Chuo kikuu cha Weill Cornell New York Marekani na MOI ulianza mwaka 2008 ambapo kwa mwaka huo Taasisi hiyo ilikuwa na madaktari bingwa wabobezi watatu tu, lakini hadi mwaka huu (2025) kuna madaktari bingwa 15 na wengine wanaendelea kupatiwa mafunzo na amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa upasuaji huo kwa kutumia akili unde ni bora na salama kabisa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa upasuaji wa Mgongo na ubongo kutoka chuo kikuu cha Weill Cornell New York cha nchini Marekani, Profesa. Roger Hartl amewashukuru watumishi wa MOI kwa ukarimu wao ambao wameendelea kumpa tangia mwaka 2008 na ameahidi kuendelea kutembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wataalam hao.

Profesa Hartl amebainisha kwamba hivi sasa ushirikiano imara uliopo baina ya MOI na Weill Cornel, unalenga kuifanya Taasisi ya MOI kuendelea kuwa kituo cha weledi cha matibabu ya Mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here