Mafanikio ya Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita 2021-2025
Dodoma
KATIKA kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Awamu ya Sita, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanikiwa kufanya mageuzi mbalimbali katika nyanja ya utafiti , upimaji wa sampuli za madini na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.

Hayo yameelezwa leo Machi, 27 2025 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST , Notka Banteze wakati akiongea na waandishi wa habari katika Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma.
Banteze amesema kuwa, mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa lengo la kuona GST inaimarika zaidi kwa ukuaji endelevu wa sekta ya madini.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya tafiti za jiolojia , jiokemia na jiofizikia amesema mpaka kufikia mwaka 2024 , utafiti wa madini ya viwandani ulikamilika ambapo jumla ya madini viwanda 44 yalibainishwa.
Sambamba na hapo, GST imefanikiwa kufanya utafiti wa madini ya helium katika mikoa ya Arusha , Manyara, Dodoma, Singida na Shinyanga na kubaini kiwango cha helium katika chemchem za majimoto zinazofaa kwa hatua ya utafiti wa kina katika maeneo ya Ziwa Natron na Eyasi.

Kwa upande wa machapisho ya utafiti , Banteze amesema GST imefanikiwa kuchapisha vitabu viwili ambavyo ni kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania toleo la tano pamoja na kitabu cha madini viwanda toleo la pili pamoja ramani za maeneo husika.
Akielezea kuhusu mafunzo kwa wachimbaji wadogo, Banteze amesema GST imekamilisha utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 2733
yaliyohusu uchukuaji wa sampuli wakilishi na utambuzi wa jiolojia ya maeneo yenye uwepo wa madini katika mikoa ya Lindi,Morogoro,Geita na Mwanza.
Banteze amefafanua kuwa, mwelekeo wa Serikali kupitia GST katika mwaka 2025/2926 kuwa, GST imepanga kufanya utafiti wa kina kw kutumia ndege ili kuongeza asilimia za utafiti wa kina kutoka asilimia 16 mpaka 34 , ikiwa na lengo la kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Amesema GST imepanga kujenga maabara ya kisasa (state of art labaoratory) katika mkoa wa Dodoma kwa ajili kuimarisha uchunguzi wa sampuli za madini nchini ili kuchochea shughuli za utafiti nchini na hivyo kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Madini.
Amesema Maabara husika itakuwa na vifaa vya kisasa na itaweza kufanya uchunguzi wa sampuli za madini nyingi zaidi ikiwemo zinazojumuisha madini muhimu na kimkakati.
Aidha, GST imepanga kujenga majengo ya kisasa ya maabara na ofisi katika mikoa ya Geita na Mbeya ili kuwasogezea huduma karibu zaidi wachimbaji madini ikiwemo wachimbaji wadogo wa madini. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza tija kwa wachimbaji wa madini kwa kuwapunguzia kuchimba kwa kubahatisha.
Pamoja na mambo mengine, Banteze amesisitiza kuwa GST imekusudia kukamilisha ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa taarifa na takwimu za Taifa za madini. Kukamilika kwa mfumo huo utaongeza ufanisi katika utunzaji na usambazaji wa taarifa za madini na hivyo kuchochea uwekezaji katika sekta ya madini.

Awali, akifungua mkutano huo mkurugenzi Idara ya Habari (Maelezo) Rodney Thadeus ameipongeza GST kwa kazi nzuri inayofanya kwa maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla katika kuelekea Dira ya Taifa ya mwaka 2050.