Home KITAIFA RAIS DK. SAMIA ANATAMBUA CHANGAMOTO ZA WENYE MAHITAJI MAALUM-MAJALIWA

RAIS DK. SAMIA ANATAMBUA CHANGAMOTO ZA WENYE MAHITAJI MAALUM-MAJALIWA

Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo Machi 24, 2025 ameshiriki futari na watoto wenye mahitaji maalum wa shule ya msingi Buigiri iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma inayomilikiwa na kanisa la Anglikana Tanzania.

Akizungumza na watoto hao Majaliwa amewaeleza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto za watu wenye mahitaji maalum na mara zote anawezesha utatuzi wake.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa watoto wenye mahitaji maalum nchini kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo yao.

“Tumieni nafasi ya kuwa hapa kusoma sana, wasikilizeni walimu wenu, wako kwa ajili yenu,”amesema.

Aidha, Majaliwa amesema kuwa Serikali inaunga mkono taasisi za dini kaunzisha maeneo ya kuwahudumia watanzania kwenye sekta mbalimbali za huduma za kijamii.

“Serikali pamoja na viongozi wa dini tunafanya kazi kwa pamoja,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kufufua vyuo sita vya watu wenye ulemavu ambavyo vilikuwa vimefungwa kwa zaidi ya miaka kumi.

Katambi amesema Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo hivyo.

“Pia Rais ametoa shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vingine vipya vya watu wenye ulemavu na tumeanza ujenzi kwenye mikoa ya Mwanza, Ruvuma na Kigoma,”amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here