Na Abdallah Nassoro- Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), mapema wiki hii inatarajia kuanza kutoa huduma za upasuaji wa ubongo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutumia roboti (brain neuro navigation) ili kuboresha ufanisi wa matibabu kwa wagonjwa.

Hayo yamebainishwa leo Machi 24, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la 11 la Wataalam wa upasuaji Ubongo na wauguzi mabingwa katika Hotel ya Protea Jijini Dar es Salaam.
Dk. Mpoki amesema kuwa kuanza kutumika kwa teknolojia hiyo kunatokana na Taasisi ya MOI kupokea msada wa kifaa tiba maalum kinachojulikana kama ‘Brain Lab’ Neuro-navigation systems kutoka chuo kikuu cha Weil Cornell New York nchini Marekani ambacho kinasaidia kuwaongoza madaktari kubaini sehemu yenye tatizo katika ubongo kwa undani wakati wa upasuaji.
“Ile ndoto yetu kama Taaisi ya MOI kuwa kituo mahiri cha masuala ya usapasuaji wa Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu inazidi kutimia, tunakwenda kufanya upasuaji kwa teknolojia ya hali ya juu sana…ushirikiano wa MOI na Weil Cornell ni wa zaidi ya miaka 16, katika kipindi chote wamekuwa wakitusaidia katika kuwajengea uwezo wataalam wetu,” amesema Dk. Mpoki.

Aidha, amesema kuwa kwa sasa asilimia 95 ya magonjwa ya ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu yanatibika taasisi ya MOI na kwamba kuanza kwa huduma hiyo mpya itapunguza asilimia tano ya wanaopewa rufaa.
“Tunatambua mchango wa chuo kikuu cha Weill Cornell, pia kwa namna ya kipekee Prof. Roger Hartl, kwa niaba ya taasisi, wizara ya afya na serikali nasema asante sana kwa ushirikiano kwa kutoa fursa kwa wataalam wetu kutoa huduma bora kwa Watanzania,” amesisitiza Dk. Mpoki.

Kwa upande wake, Daktari bingwa na mbobezi wa ubongo kutoka Chuo kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani, Profesa Roger Hartl, ameishukuru MOI kwa kutambua mchango wake na kumpatia tuzo na kuahidi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuwapa ujuzi madaktari wauguzi na wataalam wengine wa afya.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo MOI, Dk. Laurent Lemeri Mchome amesema ushirikiano baina ya taasisi hizo umewesha wataalam wazawa kupata fursa za kusomea udaktari bingwa katika fani ya ubongo nchini Marekani.

Mratibu wa kongamano hilo Dk. Hamisi Shabani amesema MOI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha Marekani, huandaa Kozi ya Kimataifa ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (Global Neurosurgery Course) kila mwaka. Kozi hiyo inalenga kuwapa mafunzo madaktari na wauguzi kuhusu mbinu za kisasa katika upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.