Dar es Salaam
KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili msanii wa uigizaji Joyce Mbaga (32), maarufu Nicole Berry na mwenzake Rehema Mahanyu (31), imetajwa leo Jumatatu Machi 24, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni.

Upande wa Jamhuri umeomba kuongezewa muda kutokana na upelezi wa kesi hiyo kutokamilika ambapo inatarajiwa kutajwa tena Aprili 14, 2025 saa nne asubuhi.
Awali washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani Machi 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu ambapo Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu aliwasomea mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira.
Katika mashitaka yao, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka matatu la kwanza la kuongoza genge la uhalifu.
Ikumbukwe kuwa Machi 17, 2025 Nicole aliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo amedhamiwa kwa hati ya nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 100 iliyotolewa na mmoja wa mdhamini wake, ambao hata hivyo majina yao hayajafahamika.