Home KITAIFA TUWAPENDE, TUWAJALI NA TUWATUNZE WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM – MAJALIWA

TUWAPENDE, TUWAJALI NA TUWATUNZE WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM – MAJALIWA

▪️Asema kwa kufanya hivyo kutawasaidia kutimiza ndoto zao

▪️Asisitiza Serikali itaendelea kufanya uwekezaji kwenye sekta ya elimu

Njombe

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wanafunzi wa shule zote nchini kuwatunza, kuwapenda na kuwajali wanafunzi wenzao wenye mahitaji maalum ili nao waweze kutimiza ndoto zao.

Ameyasema hayo leo, Jumamosi Machi 22, 2025 alipotembelea Shule ya Sekondari ya Mkoa ya Wasichana ya Njombe iliyoko Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe.

Amesema Serikali imejenga miundombinu bora ambayo sasa inawawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kusoma na kufaulu na kupata nafasi katika shule mchanganyiko na hivyo ni wajibu wa wanafunzi wengine kuwapenda na kuwasaidia.

“Nimevutiwa namna mnavyowajali na kuwapenda wanafunzi wenzenu wenye mahitaji maalum, ninaomba muendelee na upendo huo muwathamini na kuwapenda ili nao watimize ndoto zao,”amesema.

Majaliwa amesema pamoja na mambo mengine ameridhishwa na ujenzi na mandhari ya shule hiyo na zaidi amevutiwa na mifumo ya TEHAMA iliyoko katika shule hiyo.

“Nimevutiwa na mindombinu ya TEHAMA iliyopo katika shule hii, wanafunzi mhakikishe mnaitunza ili iwe na tija na kutimiza malengo yenu ya kujisomea,”amesema.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa katika shule za wasichana kwa kujenga shule kubwa zenye viwango mikoa yote nchini ikiwa ni maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya elimu na hakika sasa tunaona matunda ya uwekezaji huo,”amesema.

Naye, Naibu Waziri OR-TAMISEMI, na Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe Festo Dugange, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa shule hiyo sambamba na miradi mingine mingi ya maendeleo ikiwemo vituo vya afya, huduma za maji na miundombinu ya barabara.

Shule hiyo imegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 4 ina vyumba vya madarasa 22, mabweni 9, bwalo na jiko pamoja na miundombinu mingineyo tayari imedahili wanafunzi 460 wa michepuo mbalimbali ya masomo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here