Home AFYA WIZARA YA AFYA YAWASILISHA VIPAUMBELE 11 VYA BAJETI 2025/26 MBELE YA KAMATI...

WIZARA YA AFYA YAWASILISHA VIPAUMBELE 11 VYA BAJETI 2025/26 MBELE YA KAMATI YA BUNGE

Dodoma

WIZARA ya Afya imewasilisha vipaumbele 11 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ambavyo ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko na magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwenye ngazi za msingi hadi Taifa.

Waziri wa Afya Jenista Mhagama amewasilisha vipaumbele hivyo leo Machi 21, 2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dk. Christine Mnzava.

“Vipaumbele hivi ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kuimarisha tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya, huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto,” amesema Waziri Mhagama.

Vipaumbele vingine amevitaja kuwa ni kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam wa Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi, pamoja na kuimarisha Tiba Utalii nchini.

Amevijata vipaumbele vingine kuwa ni kuendeleza na kusimamia afua za tiba asili na tiba mbadala, kuimarisha upatikanaji wa huduma za tiba dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko.

“Maeneo mengine ya kimkakati ni kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu wa kudumu,” amefafanua Mhagama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here