Home KITAIFA NACTVET YAWAHAKIKISHIA WADAU USIMAMIZI THABITI WA UBORA WA ELIMU YA UFUNDI NA...

NACTVET YAWAHAKIKISHIA WADAU USIMAMIZI THABITI WA UBORA WA ELIMU YA UFUNDI NA AMALI

Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeelezea dhamira yake kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi na yale ya amali yanayotolewa kwenye vyuo na shule za sekondari za ufundi nchini yanazingatia viwango na ubora ili kuzalisha wahitimu wanaokubalika katika soko la ajira.

Hayo yameelezwa Machi, 19 2025 jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dk. Mwajuma Lingwanda, wakati akichangia mada kuhusu mchango wa wahitimu wa ufundi stadi katika maendeleo ya jamii na uchumi, kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Amesema matarajio ya Serikali ni kuwa na wahitimu wa ufundi na amali watakaochangia kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kupitia ujuzi walioupata. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanyika tafiti za mara kwa mara katika sekta ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuwezesha uandaaji wa mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji mafunzo kulingana na mahitaji ya viwanda na soko la ajira kwa ujumla.

“Tafiti za mara kwa mara zitasaidia kutoa taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya soko la ajira na kutoa mrejesho kuhusu wahitimu wa ufundi, hivyo kuboresha utoaji mafunzo kwenye vyuo vyetu,” amesema Dk. Mwajuma.

Dk. Mwajuma amewahakikishia wadau kuwa NACTVET itaendelea kushirikiana nao katika kuimarisha utoaji mafunzo ya ufundi na kuzalisha wahitimu wenye sifa watakaoweza kuajirika na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here