▪️Asema Tanzania inayo teknolojia ya uchakataji mazao ya misitu.
▪️Aisistiza Wizara kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji wa mazao ya misitu.
Njombe
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa uzalishaji mazao ya misitu kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao hayo hapa nchini badala ya kusafirisha malighafi hizo nje ya nchi.

Ameyasema hayo leo, (Ijumaa 21, Machi, 2025) katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Njombe.
Amesema kuwa Tanzania kwa sasa inayo teknolojia kubwa ya uchakataji wa mazao ya misitu na utengenezaji wa Samani zake hivyo hakuna haja ya wadau wa misitu kusafirisha mazao hayo kwenda nje kwa ajili ya uchakataji.

“Lazima tuweke ukomo wa uvunaji na uchakataji tunataka kila kitu wamalize hapa hapa kama wanavyofanya TANWAT, wanaanza mwanzo mpaka mwisho wakiwa hapa hapa Tanzania, hapa hapa njombe kwa hivyo na viwanda vingine vibainishwe ambavyo havijakamirisha, tulishawapa muda inatosha,”amesema.

Aidha, Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika kuanzisha mashamba ya miti na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu.
Pia ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na Mamlaka nyingine kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu kuhusu uhifadhi na biashara ya kaboni ili waweze kuanza kunufaika kupitia biashara hiyo.

“Taasisi za misitu ziweke mipango thabiti ya kukabiliana na uchomaji moto ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia teknolojia katika kutambua na kupambana na moto,”amesema.
Pia amezitaka, Wizara na Taasisi hizo kuhakikisha zinaboresha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa sekta ya misitu na jamii inayozunguka maeneo ya misiti ili kuhakikisha mipango na mikakati ya uhifadhi inatekelezwa kwa ufanisi.

“Wataalamu wa misitu wanapaswa kushirikiana na jamii katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi, ikiwemo kuanzisha mashamba ya misitu, na programu za upandaji miti,”amesema.
Awali, Majaliwa alitembelea kiwanda cha uchakataji mazao ya misitu cha TANWAT (Tanganyika Wattle Company Limited) kilichopo Njombe mjini ambapo alishuhudia shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.