Home UCHUMI GAVANA TUTUBA: UCHUMI WA TANZANIA UNAENDELEA KUIMARIKA

GAVANA TUTUBA: UCHUMI WA TANZANIA UNAENDELEA KUIMARIKA

Dar es Salaam

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa,hali ya uchumi wa Tanzania imeendelea kuimarika na kuwa himilivu.

Gavana Tutuba ameyasema hayo Machi, 20 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa wananchi na wadau mbalimbali.imefanyika makao makuu ya BoT jijini Dodoma, makao makuu ndogo Zanzibar, matawi ya Mtwara, Mwanza,Arusha na Mbeya.

“Mpaka sasa, Tanzania imeendelea kung’ara katika medali za kiuchumi kidunia. Hali yetu ya uchumi, imeendelea kuwa nzuri katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Fedha ambayo imeendelea kuimarika, imeendelea kuwa na utulivu, imeendelea kuwa thabiti.

“Imeendelea kuwa na mtaji mkubwa na ukwasi wa kutosha na pia ina ufanisi mzuri wa viwango vya kimataifa na inajiendesha kwa faida na inaendelea kukuwa kwa

Amesema, kwa kipindi cha miaka mitatu Sekta ya Uchumi na Fedha nchini imeendelea kufanya vizuri.

“Na kwa takwimu tunafahamu kwamba, kwa mwaka 2024 uchumi wa nchi yetu ulikuwa kwa takribani asilimia 5.4 ikilinganishwa na ukuwaji wa uchumi wa kidunia ambao ulikuwa asilimia 3.2.Kwa hiyo tumefanya vizuri.”

Aidha, kwa upande wa mfumuko wa bei, Gavana Tutuba amesema ulikuwa asilimia 3.1 ukilinganishwa na mfumuko wa bei wa kidunia wa asilimia 4.7.

Mikopo

Kwa upande wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, Gavana Tutuba amesema, mambo yalikuwa mazuri, kwani likuwa kwa asilimia 16.8 ikilinganishwa na lengo la asilimia 15.

“Lakini, pia kwa upande wa mikopo chechefu tumeendelea kufanya vizuri ambapo kiwango cha mikopo chechefu kwa mwaka 2024 ilikuwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika kimataifa cha asilimia 5.Kwa maana hapa nako tumefanya vizuri,”amesema

Vilevile amesema, nakisi ya urari ya malipo nje ilipungua kufikia asilimia 2.7 ya pato la taifa kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 3.7 ya pato la Taifa kwa mwaka 2023.

“Akiba ya fedha za kigeni imefikia dola za kimarekani milioni 5.5 kiwango ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa miezi 4.7,”ameongeza.

Mbali na hayo amesema, Pato la Taifa limeendelea kuwa himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Amesema, kwa mwaka 2024 ilikuwa takribani asilimia 41.1 pato la taifa kwa thamani halisi ya sasa.Ukilinganisha na ukomo uliowekwa kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa asilimia 53.

“Kwa hiyo, takwimu hizi ni kiashiria tosha kwamba tunafanya kazi vizuri na Mwenyezi Mungu ameendelea kutubariki kama nchi ya Tanzania uchumi bado upo vizuri na tunaendelea vizuri,”amesema.

Huduma za Kifedha

Gavana Tutuba amesema, katika kipindi cha karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la huduma za kifedha hapa nchini ambapo ongezeko hilo limechangiwa na kasi, usimamizi mzuri wa Sekta ya Fedha pamoja na kuongezeka kwa watoa huduma ndogo za fedha hasa baada ya kupitishwa kwa sheria ya usimamizi wa huduma ndogo za fedha ya mwaka 2018.

Amesema, licha ya mafanikio hayo bado zipo changamoto chache zilizojitokeza katika sekta hiyo.Miongoni mwa changamoto hizo katika huduma za kifedha,G ni pamoja na utolewaji wa mikopo isiyofuata sheria (mikopo umiza au kausha damu).

Sambamba na wanaotoa mikopo yenye riba kubwa huku wengine wakitoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni.

“Wengine walikuwa wakitoa huduma hizo kwenye mitandao ikiwemo utapeli uliofanyika kwenye shughuli za upatu,”amesema.

Akizungumzaia kuhusu Upatu

Kutokana na changamoto hiyo, Gavana Tutuba ametoa wito kwa wananchi wote kujiepusha na shughuli za upatu.

Pia, amewataka wananchi kuhakikisha wanapata huduma za mikopo kwa watoa huduma wenye leseni halali kutoka Benki Kuu au kupitia taasisi zilizokasimishwa mamlaka.

“Kwenye halmashauri kwa leseni za VICOBA na kwenye Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa leseni za SACCOS,”amesema.

Pia, amewataka watoa huduma za mikopo wenye leseni kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na ambazo haziwaumizi wananchi.

Amesema, kwa yule ambaye atakwenda kinyume na leseni yake, Benki Kuu itachukua hatua ikiwemo kumfutia leseni husika.

Kuhusu mfungo

Gavana Tutuba amesema, kwa upande wa kiroho, viongozi wengi wa kidini zote za Kiislamu na Kikristo wameendelea kufundisha hiki ni kipindi muhimu ambacho mwanadamu anapaswa kumrejea Mungu wake.

“Kipindi hiki cha mfungo ninafahamu ni kipindi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu na kipindi ambacho kina faida nyingi za kiroho na kimwili. Ni kipindi ambacho kinatupatia fursa na Mwenyezi Mungu kwa sala, maombi na hata kutafakari ukuu wa Mwenyezi Mungu,”amesema.

Pia, amesema katika kipindi hiki kila mmoja anapata fursa ya kutakasa roho na nafsi yake.

Gavana Tutuba amebainisha kuwa, kunaimarisha afya ya moyo na kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo ugonjwa wa saratani.

Amesema,matarajio yake ni kwamba katika kipindi hiki kitaendelea kuleta chachu ya kuimarisha amani, upendo na mshikamano kuanzia ngazi ya familia,Taifa hadi Kimataifa.

“Kwa hiyo, tuendelee kutumia kipindi hiki kujitafakari na kuangalia namna ya kumrudia Mwenyezi Mungu.”

Pia, Gavana Tutuba amewahimiza kila mmoja kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kulinda amani iliyopo.

Mufti wa Tanzania

Naye Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber Bin Ally, ameitaka Benki Kuu kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya huduma za fedha.

Amesema, kupitia elimu ya fedha kwa wananchi itawapa uwanda mpana wa kuweza kutambua sehemu sahihi za kupata mikopo.

Pia, amesema elimu hiyo itasaidia wananchi kuendesha biashara zao kwa faida.

“Kwa hiyo msiache kutoa elimu hii, ili iweze kufikia mahali ambapo mwananchi anaweza kufanya shughuli zake kwa utulivu.

Pia,amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani nchini hasa kipindi hiki Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

“Kwa hiyo, Watanzania tushikamane tuitunze amani,”amesema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here