Home KITAIFA NI MAONO YA DK.SAMIA WANANCHI WOTE WAPATE UMEME – KAPINGA

NI MAONO YA DK.SAMIA WANANCHI WOTE WAPATE UMEME – KAPINGA

📌 Asema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani Vijiji 4000 havikuwa na umeme

📌 Aitaka TANESCO na REA kuendelea kutoa elimu ya kuunganisha umeme

📌 Nishati ya umeme yauongezea ufanisi Zahanati ya Mang’oto

Njombe

NAIBU Waziri NishatiJudith Kapinga amesema ni maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuona wananchi wote wanapata huduma ya umeme.

Kapinga ameyasema hayo leo Machi 17, 2025 katika Kijiji cha Mang’oto Wilaya ya Makete mkoani Njombe wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Rais legacy yake na maono yake ni Tanzania nzima mijini, vijijini na vitongojini kupata umeme, ndio maana mnamuona anahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya umeme kwenye Vitongoji,” amesema Kapinga.

Ameongeza kuwa mwaka 2020 Serikali iliahidi kuvifikishia umeme vijiji vyote 12,318 ifikapo Desemba 2025 na wakati Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani takribani Vijiji 4000 havikuwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

Katika hatua nyingine Kapinga amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi pamoja na utoaji wa elimu wa jinsi ya kufanya maombi ya kuunganisha umeme.

Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa kutumia namba 180 ambayo haina malipo kwa mteja

Kapinga amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha umeme wa uhakika na unaotabirika unawafikia wananchi wote ili waweze kunufaika kwa shughuli za kiuchumi.

Kufika kwa umeme katika Kijiji cha Mang’oto kumewanufaisha wananchi ambapo wamefungua shughuli za kiuchumi ikiwemo mashine za kusaga nafaka lakini pia kuweza kurahisisha huduma katika Zahanati ya Mang’oto ambayo hapo awali ilikuwa ikitumia umeme wa jua.

Kutokana na hilo wananchi wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini kwani wameweza kuinua vipato vyao ikiwemo kufungua biashara kama za kuchomelea na kuboresha huduma za afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here