Lindi
MBUNGE wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakazi wa Wilaya ya Ruangwa hawana deni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wilayani humo.

Amesema Rais Dk. Samia ametoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo.
Ameyasema hayo leo Jumamosi, 15 Machi 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wanakijiji wa kijiji cha Narungombe, Wilayani Ruangwa.
“Rais Dk. Samia amewezesha kupatikana kwa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo kwenye wilaya yetu ya Ruangwa, Tunaachaje kumuunga mkono kwa kazi kubwa aliyoifanya,”amesema.

Amesema Wana-Ruangwa wanatoa shukrani za dhati kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
“Wilaya yetu ilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kutokana na kuwa na chumvi nyingi chini inayotokana na sababu za kijiografia lakini Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana,”amesema.
Amesema Serikali iko katika hatua za utekelezaji za mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 119 kutoka mto Nyangao, kuja vijiji 34 vya Ruangwa ambao utahakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika wilayani humo.

“Nitaendelea kufanya kazi na nyie usiku na mchana, jua kwa mvua hadi kuhakikisha Ruangwa inafanikiwa zaidi,”ameongeza.
Katika Hatua nyingine, Majaliwa ameshuhudia wanachama 24 wa Chama cha ACT Wazalendo wakijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Miongoni mwa wanachama hao ni pamoja na Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Wilaya ya Ruangwa, Hammis Selemani Chikanga, Diwani wa Kata ya Mbwemkuru Ismail Ali Mbwerei, Katibu wa Vijana Omary Kitunguu, pamoja na wanachama wengine.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Wilaya ya Ruangwa Hammis Chikanga, Amesema sababu za wao kujiunga na CCM ni kuunga mkono jitihada na kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia inafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi na inaleta miradi na mambo mengi kwa wananchi hivyo tukiendelea kuwapinga na kuwakosoa tutakuwa hatuwatendei haki,”amesema.