Dar es Salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imetoa elimu kuhusu ugonjwa ya figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa walimu wakuu wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam pamoja na polisi kutoka Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya ya kiungo hicho.

Akizungumza leo Machi, 14 2025 kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Faraja Chiwanga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku hii ni kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya ya figo, ikiwa ni pamoja na njia bora za kujikinga na magonjwa sugu ya figo ambayo yanatajwa kuwa tishio kwa jamii.
“Tunatumaini kuwa walimu hawa wataweza kufikisha elimu hii kwa wanafunzi wao, hivyo kuwajengea msingi wa afya bora ya figo tangu wakiwa vijana. Watakuwa mabalozi na wahamasishaji wakubwa wa afya ya figo katika familia zao, jamii zao, na hata maeneo yao ya kazi,” amesema Dk. Faraja.

Naye Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dk. Jonathan Mngumi, ameeleza kuwa ugonjwa wa figo unawaathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 40-50, ambao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya jamii na hii inaonesha changamoto kubwa katika kupambana na ugonjwa huu, hasa kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za afya.
Nao Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ralph Meela na Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Sekondari Dk. Mavumba Hussein wameushukuru uongozi wa MNH kuwapa elimu hiyo na kusema watakua mabalozi wazuri sehemu zao za kazi na jamii inayowazunguka.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 7% ya watu nchini Tanzania wanaugua ugonjwa sugu wa figo huku idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya uchujaji wa damu ikitajwa kuongezeka kutoka 380 mwaka 2014/2016 hadi 2900 mwaka 2021/2022, na sasa wagonjwa wanaopatiwa huduma hiyo ni 3500. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “JE FIGO YAKO IKO SALAMA? Tutambue mapema, ilinde afya ya figo yako”.