Home KITAIFA VIJANA WENYE ELIMU YA DINI NI NGUZO MUHIMU YA MAENDELEO-MAJALIWA

VIJANA WENYE ELIMU YA DINI NI NGUZO MUHIMU YA MAENDELEO-MAJALIWA

Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema vijana wenye elimu na maarifa ya dini ni nguzo muhimu ya ustawi na maendeleo katika jamii kwani imani imara ya kidini hujenga jamii zenye maadili mema, ufanisi katika kazi, na upendo wa dhati kwa kila mmoja.

Pia, amesema Serikali ina matarajio makubwa kwa vijana wanaoshiriki mashindano Quran kwani kwa kutumia maarifa na ujuzi wanaoupata katika mashindano hayo kutekeleza majukumu muhimu ya kijamii na kiroho.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 8, 2025 alipozungumza na wananchi katika Mashindano ya 16 ya Kuhifadhi Quran Tukufu ngazi ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi, Dar es Salaam.

“Mashindano haya ni fursa ya kukuza imani na maarifa yenu. Kuhifadhi Quran ni jambo lenye manufaa mengi kwani inaimarisha uhusiano wenu na Mwenyezi Mungu na inajenga msimamo wa kiroho. Nina hakika mnapokuwa na imani imara, nidhamu, na maadili mazuri baadaye mtakuwa viongozi bora wa familia, jamii, na Taifa kwa ujumla,”amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mashindano hayo yana mchango mkubwa katika kuimarisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi, pia yanachangia katika kukuza sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi na utalii kwani kila mwaka washiriki kutoka mataifa mbalimbali wanakuja nchini kushiriki au kushuhudia mshindano hayo.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mashindano ya kuhifadhi Quran, Waziri Mkuu amesema mashindano hayo yana manufaa kwa washiriki na kwa Taifa kwani yanawawezesha washiriki kuwa na uwezo wa kuhifadhi na kuelewa mafundisho ya Quran Tukufu.

“Kupitia mashindano haya, tunawahamasisha vijana wetu kuwa na moyo wa kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa juhudi kubwa,”amesema.

Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuipongeza taasisi ya Mana’Hil AL – Irfan kwa juhudi zao kubwa katika kuandaa mashindano hayo.

“Uwezo wa kuwa na mashindano haya kwa miaka 16 mfululizo ni dalili ya dhamira thabiti ya kuwahamasisha vijana wetu katika kuzingatia na kuhifadhi Quran Tukufu na kuhakikisha kwamba tunalinda utamaduni wa dini, maadili na imani ya Kiislamu,”ameongeza.

Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali inaunga mkono taasisi zote zinazojitahidi kuinua elimu ya dini na maadili, kwa lengo la kuwa na Taifa lenye vijana bora, wenye imani thabiti na maadili mema.

Pia,Majaliwa ametoa wito kwa viongozi dini waendelee kuliweka suala la kudhibiti mmomonyoko wa maadili kuwa ajenda ya kudumu katika vikao na mikutano yao.

“Ninawasihi sana endeleeni kukemea vikali vitendo vyote ambavyo vinamchukiza Mwenyezi Mungu na ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania,”amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here