Home KITAIFA MTUHUMIWA MMOJA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI ARUSHA.

MTUHUMIWA MMOJA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI ARUSHA.

Arusha

JESHI la Polisi Mkoani Arusha linamshikilia mtu mmoja aitwaye Emmanuel Charles (25) mkazi wa wilaya ya Arumeru kwa tuhuma za mauaji ya binti mmoja (17) ambaye jina lake limehifadhiwa mkazi wa wilaya ya Arumeru na mkoani humo.

Akitoa taarifa hiyo leo Machi, 6 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP, Justine Masejo amesema mtuhumiwa huyo alitenda tukio hilo Machi 01 mwaka huu kwa kumjeruhi marehemu na kitu chenye ncha kali na kisha kumbaka.

Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa marehemu alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha.

Aidha amesema upelelezi wa tukio hili unaendelea na pindi utakapokamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata.

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la kifo cha mtoto wa miezi 11 jina limehifadhiwa mkazi wa Olasiti Jijini Arusha ambaye alifariki dunia Machi, 4 mwaka huu.

SACP Masejo amebainisha kuwa pindi uchunguzi huo utakapokamilika watatoa taarifa zaidi. Aidha mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari, tayari umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajiili ya taratibu za mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, pia limesema litaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuwakamata watu wote watakaobainika kujihusisha na uhalifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here