Home KITAIFA RAIS DK. MWINYI: UNESCO KUSAIDIA ZANZIBAR KUENDELEZA UCHUMI WA BULUU

RAIS DK. MWINYI: UNESCO KUSAIDIA ZANZIBAR KUENDELEZA UCHUMI WA BULUU

Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amelishauri Shirika la Elimu , Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa ( UNESCO) kuisaidia Zanzibar kuendeleza Uchumi wa Buluu kwani ni sekta muhimu kwa uchumi na ustawi wa wananchi wake.


Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo Machi, 5 2025 alipozungumza na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu Audrey Azoulay waliofika Ikulu kuonana naye.

Ameelezea ujumbe huo kuwa kwa sasa sekta ya uchumi wa buluu ndio kipaumbele cha Serikali inayohitaji kupewa msukumo wa ziada wa misaada ya kitaalamu,Teknolojia na fedha ili kuwa endelevu na kuiwezesha nchi kunufaika na Rasilimali za kutosha ziliomo baharini.

Amefafanua kuwa uchumi wa buluu una fursa nyingi zinazoweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo na ukuaji wa Uchumi, fursa za ajira na kuimarisha maisha ya wananchi na kuishauri UNESCO kuwa tayari kushirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo.

Rais Dk. Mwinyi amelitaka Shirika hilo kuongeza misaada zaidi kwa Mendeleo ya Mji wa Urithi wa Kimataifa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni kitovu cha Utalii wa Zanzibar na eneo jengine muhimu kwa Uchumi na ukuaji wa sekta ya Utalii kutokana na kutembelewa na idadi kubwa ya Watalii wa kutoka Mataifa mbalimbali duniani kila siku.

Amesema bado zipo changamoto nyingi katika kuuendeleza mji mkongwe ili ubaki katika haiba na urithi wake kutokana na kuwa na idadi kubwa ya nyumba zinazohitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, Udhibiti wa uingiaji na utokaji wa Magari unaopaswa kubadilika kulingana na Mazingira ya sasa ndani ya Mji Mkongwe bila kuathiri Maisha ya wakaazi wa Mji huo.

Amesema suala la mji huo linahitaji kuungwa mkono na Wadau wengi zaidi ikiwemo sekta binafsi na Washirika wa Maendeleo na kuahidi Serikali kuwa tayari kushirikiana nao kikamilifu.

Rais Dk.Mwinyi ameishauri UNESCO kuwa na Utaratibu sahihi na wa haraka juu ya suala zima la Mashauriano kati ya pande mbili inapotokezea suala la Ukarabati wa Majengo yalioyomo ndani ya Mji huo.

Akizungumzia Hifadhi ya Msitu wa Jozani Dk. Mwinyi amesema ni eneo muhimu linalohitaji uhifadhi bora unaozingatia mazingira endelevu na ustawi wa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi hiyo na Watalii wanaoitembelea na tayari Serikali ina makubaliano maalum na Wananchi ya kulinda na kuuifadhi Msitu huo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay ameihakikishia Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo katika juhudi za kuleta Maendeleo endelevu katika sekta tofauti na ustawi wa watu wake na kusisitiza kuwa shirika hilo liko tayari kuchukua juhudi maalum na misaada ya kitaalamu ,teknolojia na Uzoefu kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu na kupongeza Mafanikio yaliofikiwa katika sekta ya elimu hapa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here