Home KITAIFA RAIS SAMIA ASIKIA KILIO CHA WANANCHI BARABARA YA SONI- BUMBULI-KOROGWE

RAIS SAMIA ASIKIA KILIO CHA WANANCHI BARABARA YA SONI- BUMBULI-KOROGWE

Tanga

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wananchi wa Bumbuli, mkoani Tanga kuhusu ujenzi wa barabara ya Soni – Bumbuli – Korogwe (km 77), kwa kiwango cha lami ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utajengwa kwa awamu.

Akihutubia wananchi wa Wilaya ya Lushoto mkoani humo katika mkutano wa hadhara leo Februari, 24 2025 Rais Samia ameeleza kuwa tarehe 06 Machi, 2025 Serikali itafungua zabuni ya kumtafuta Mkandarasi wa kujenga barabara hiyo.

Dkt. Samia amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanzia Soni- Bumbuli (km 22) na Kwameta – Kwashemsi (Km 9.3).

“Barabara hii mwanangu January (Mbunge wa Bumbuli) amekuwa akiililia sana, baada ya kusikia kilio chake basi nikasema tangazeni, tarehe 6 mwezi ujao tunafungua tenda kutafuta mkandarasi,” amesema Dk. Samia.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo (km 218.2) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba amemshukuru Rais Dk. Samia Skwa kutoa kibali cha barabara hiyo kutangazwa ambayo itakuwa mkombozi na kiuganisha kati ya Bumbuli na Korogwe Mkoani Tanga.

Rais Dk.Samia anaendelea na ziara yake mkoani Tanga ambapo leo ameweka jiwe la msingi la ufunguzi wa jengo la Halmashari ya wilaya ya Bumbuli na kuzungumza na wananchi wa wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here