Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali Itaendelea na mikakati mbalimbali kuhakikisha inawekeza kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa zaidi ya maendeleo hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo Februari, 22 2025 alipozindua Hatifungani ya ZANZIBAR SUKUK, VIwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar.
Amefafanua kuwa Serikali imeamua kwa makusudi kuwa na utaratibu wa Hati Fungani kuwa njia rasmi ya kuyafikia maendeleo endelevu hivyo SUKUK itaenda Kufanikisha azma hiyo.
“Serikali imepanga kutekeleza Miradi mingi katika Muda Mfupi ujao hivyo kuwepo kwa ZANZIBAR SUKUK kutaipa Serikali uwezo na uhakika wa kupata fedha za utekelezaji wa miradi hii,” amesema.

Dk.Mwinyi amebainisha kuwa Nchi nyingi Zilizoendelea Duniani zimefanikiwa kwa kupitia Mfumo huo wa SUKUK unaozingatia Misingi ya Sharia.
Ameeleza kuwa lengo ni kuimarisha uwezo wa Zanzibar kiuchumi na kuwasisitiza wananchi ,Wadau na Taasisi za Umma na Binafsi kuchangamkia fursa hiyo inayompa mdau faida ya asilimia 10.5 kila Mwaka kuwa njia muhimu ya kujiimarisha kiuchumi.

Rais Dk.Mwinyi amesema kuwa mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayofanyika hivi sasa hapa nchini yanafanyika kufuatia kiu kubwa walionayo wananchi na uhitaji wa nchi katika maendeleo.
Pia amesema mafanikio ya hatua hiyo yanahitaji ushiriki wa wananchi wengi watakaonunua Hatifungani za ZANZIBAR SUKUK na kuwahakikishia kuwa ipo katika hali nzuri.

Amesisitiza kuwa utaratibu huo utaweka usalama na utulivu wa sekta ya fedha nchini.
Rais Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kukanusha taarifa Potofu zinazosambazwa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuwa serikali inakusudia kuiuza Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ.

Ameeleza kuwa Kinachofanyika ni kuijengea uwezo benki hiyo ili iwe na mtaji mkubwa zaidi wa kuikopesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hizo.