Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kumaliza Matatizo ya kiafya wanayokabiliana nayo Wananchi Wanaoishi katika Visiwa Vidogovidogo kwa kufikishwa katika Matibabu kwa wakati ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika ikiwemo vya akinamama na watoto.

Rais Dk.Mwinyi ametoa tamko hilo baada ya kuzindua Boti za kubeba Wagonjwa wakati wa dharura hafla iliofanyika Verde Mtoni , Wilaya ya Mjini.
Amefafanua kuwa Boti hizo ni sehemu ya uimarishaji wa huduma za dharura na mfumo wa wa rufaa kwa wagonjwa wanaotoka kwenye Visiwa wanaopewa rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali za Wilaya, Mkoa na Taifa.

Dk.Mwinyi ameiagiza wizara ya afya kuandaa utaratibu mzuri wa matumizi ya boti hizo ikiwemo matengenezo ya mara kwa mara iinapohitajika ili kuhakikisha zinafanya kazi muda wote kufikia lengo lililokusudiwa.
Ameeleza kuwa serikali imeamua kuzipeleja boti hizo katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi na kwengine kutafanyiwa utaratibu wa
Haraka baadae.

Aidha ametoa rai kwa wananchi kutumia huduma hizo kwa taratibu zilizowekwa na wizara ya afya na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa dharura yoyote inapotokea ili waweze kuwasaidia kwa haraka kupunguza madhara yanayoweza kuepukika.
Dkt, Mwinyi ameishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia gharama za ununuzi wa boti tano ambazo tatu tayari zimekamilika na mbili zitakamilika muda mfupi ujao.

Akizungumza katika Uzinduzi huo Meneja wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Ernest Massiah amesema boti hizo zitaweka utofauti baina ya uhai na kifo na kuchochea dhamira ya Zanzibar kuwa kituo pekee tiba na matibabu kinachotambulika Kimataifa na kuahidi kwa Benki ya Dunia kuendelea kuisaidia Zanzibar.
Naye Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amewahakikishia Wananchi wanaoishi katika visiwa huduma za uhakika zitakazoanza hivi karibuni na kuwa tayari kuzitumia huduma hizo hususan akina Mama na watoto.

Boti hizo zimegharimu takribani Shilingi bilioni 2 na zimetengenezwa na Kampuni ya QIRO GROUP LIMITED.