Dar es Salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi mpya ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kusimamia kwa umakini ufadhili wa masomo katika masomo ya elimu ya juu ya teknolojia ya nyuklia, ufadhili uliopewa jina la ‘Samia Scholarship Extended Program.

Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Februari, 19 jijini Dar es Salaam, wakati akizindua bodi mpya ya TAEC, na kusisitiza taasisi hiyo kuzidi kutenga fedha kwa ajili ya ufadhili wa ‘Samia Scholarship Extended Program’ ambao huwawezesha watanzania kusoma nje ya nchi fani mbalimbali zinazohusu mambo ya atomu na nguvu za nyuklia.
Amesema ni muhimu kutengeneza ushirikia huo ili kuweza kupata wanafunzi ambao watasaida kupata watalaam wenye weledi katika fani ya atomu na nguvu za nyuklia.
“Nawashauri bodi mpya ya TAEC kuimarisha uhusiano wenu na vyuo vikuu vinavyojihusisna na masuala ya sayansi hasa katika utafiti ili kuweza kupata wanafunzi Bora watakaopata ufadhili,”amesema Profesa Mkenda.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya TAEC Profesa Joseph Msambichaka amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwakumuacha aendelee kushikilia jukumu hilo na kuahidi kuyatekeleza kama inavyopaswa.
Amesema katika kipindi chote atakachoendelea kushika nafasi hiyo atatoa ushirikiano kuhakikisha Taasisi hiyo inafanya kazi kwa mujibu WA sheria.

“Hii ni heshima kubwa sana kwangu na naahidi nitatekeleza majumu yangu kadri nitakavyoweza,”amesema Profesa Msambichaka.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Profesa Najat Mohammed alisema wataendelea kudhibiti na kuhakikisha wanakuwa makini katika matumizi ya atomiki.