▪️Asema Serikali ilifuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo.
Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetumia shilingi trilioni 8.2 kugharamia wanafunzi tangu ilipoanzishwa.

Amesema kuwa pia katika kipindi hicho wanafunzi takribani 830,000 wamenufaika na mfumo huo wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo.
Amesema hayo leo Februari 17, 2025 alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Mafanikio tuliyonayo leo, ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na michango ya viongozi wetu. Viongozi wetu katika awamu zote walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri, viongozi wetu walioona mbali kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo,”amesema.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.5.

“Ninatambua marejesho hayo yamepatikana kutokana na jitihada na ubunifu mkubwa ambao unasaidia kuwafikia wanufaika ambao wamehitimu na mikopo yao imeiva,”amesema.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu haiwi mzigo kwa Wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo.

“Kwa sasa mnufaika anarejesha kiasi kile kile ambacho amekopeshwa kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha ongezeko la madeni ya mikopo hiyo,”amesema.
Majaliwa ameiagiza Bodi ya Mikopo kuendelea kuweka mikakati ya kuendana na kasi ya mababiliko ya teknolojia na ifanye maboresho ya kujiunganisha na kuzungumza lugha moja na taasisi za fedha nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani alikuta fedha zinazotolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 464.

“Lakini alipoingia aliagiza fedha kwa ajili ya mikopo ziongezwe, na tuliongeza hadi kufikia bilioni 570, tukaendelea hadi bilioni 654 na sasa ni shilingi bilioni 73,”amesema
Ameongeza kuwa Rais Dk. Samia katika kuhakikisha kada za Sayansi zinaendelea kupewa kipaumbele ili kuzalisha wataalam wengi zaidi, aliiagiza Wizara ya Elimu kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kutoa ufadhili kwa ajili ya kada hizo ambayo tuliita Samia Scholarship.
“Wakati tunaanza tulitoa shilingi bilioni 3 kama majaribio, baadae tulitoa bilioni 6 na sasa hivi tumetoa shilingi bilioni 8.9,”amesema.