Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea Kuunga mkono Harakati za Jumuiya ya Wawakilishi Wanawake (UWAWAZA) za kuwajengea Uwezo Wanawake katika Maendeleo yao kisiasa,Kiuchumi na Kijamii.

Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo Februari, 17 2025 lalipozungumza na Wajumbe wa jumuiya hiyo waliofika Ikulu kujitambulisha na Kumpongeza Dk.Mwinyi.
Ameeleza kuwa Jumuiya hiyo ni sauti muhimu katika kupigania haki za Wanawake ndani na Nje ya Baraza la Wawakilishi na kuahidi kuendelea kuiunga Mkono kuyafikia Malengo yao.
Ameeleza kufarijika na kazi zinazofanywa na Jumuiya hiyo za kuimarisha Ushiriki na kuongeza Idadi ya Wajumbe Wanawake katika Baraza la Wawakilishi kwani Uzoefu unaonesha wanawake wanafanya vizuri katika uongozi.

Rais Dk.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha Wanawake Kutosita kugombea nafasi za Uongozi katika Uchaguzi ujao ili kuongeza Idadi yao katika Baraza la Wawakilishi.
Ametoa ushauri kwa UWAWAZA kufanya tathmini ya Miaka 22 tangu Kuanzishwa kwake ili kubaini maeneo muhimu yanayohitaji Msukumo wa Serikali kuwainua Wanawake , Kisiasa , Kiuchumi na kijamii.

Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wajumbe hao kuendelea kutoa nafasi zaidi kwa Wanawake kwani Wale aliowapa dhamana katika Sekta Mbalimbali Wanaendelea kufanya vizuri.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawakilishi Wanawake Saada Mkuya Salum amempongeza Dk. Mwinyi kwa mafanikio ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, masoko ,hospitali na vituo vya afya ambavyo vimekuwa nyenzo muhimu kwa ustawi wa wanawake.

Ameeleza kuwa jumuiya hiyo hivi sasa ina mkakati maalum wa kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanaingia Baraza la Wawakilishi kuongeza nguvu ya kutetea haki na ustawi wao.