▪️Asisitiza Rais Dkt. Samia tunaye na tunaenda naye.
▪️Asema Rais Samia ni mgombea aliyejipambanua kwa uhodari na uimara wake kiutendaji
▪️Amtaja Dkt. Nchimbi kuwa kiongozi mchapakazi na anatosha kwenye nafasi ya ugombea mwenza.
Simiyu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshamaliza mchakato wa kupata mgombea Urais wa Chama hicho katika uchaguzi Mkuu utakaofanya mwaka 2025.

Ametoa kauli hiyo leo Februari 15, 2025 wakati Mkutano Mkuu Maalum Chama cha Mapinduzi Jimbo la Itilima, uliofanyika katika uwanja wa Stand Mpya ya Itilima, mkoani Simiyu.
Majaliwa amesema kuwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi chama hicho kimewapa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia Watanzania katika kipindi cha 2025-2030.
“Mama yupo na sisi, tunaye na tunaenda nae, Mwaka huu tumewaleta wagombea bora kabisa ambao wamethibitisha bila shaka kwamba utendaji wao umetukuka katika kipindi walichokuwa wanawatumikia watanzania,”amesema.

Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia imeshuhudiwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imegusa moja kwa moja maisha ya Watanzania kwenye sekta za elimu, kilimo, afya, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Chama cha Mapinduzi kina Sera imara zinazotekelezeka na watanzania wanakiamini Chama cha Mapinduzi, kinakubalika na ndicho kinachotumainiwa kutokana na uwezo wake wa hali ya juu wa kuwatumikia Watanzania, Mwaka huu tunalojukumu la kuwaambia watanzania nini tumefanya na nini tutafanya katika kuwajibika q ww wa na kusimamia maendeleo ya Watanzania,”amesema.

Kwa Upande wake, Mbunge wa jimbo la Itilima Silanga Njalu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoomgozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeipatia Wilaya ya Itilima takribani shilingi bilioni 85 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akitolewa mfano kwenye sekta ya Maji Njalu amesema kuwa Rais Dk. Samia aliridhia kutoa kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuanzisha miradi midogo midogo ya maji.
“Alifanya hivi wakati utekelezaji wa mradi wa maji kutoka ziwa victoria ukiendelea,”amesema.

Ameongeza kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Dk. Samia ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya utoaji wa pembejeo na utaalam kwenye sekta ya kilimo.
“Pia tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 41 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme,”amesema.