Dar es Salaam
ASASI za Kiraia kutoka nchi za Maziwa Makuu zimeshauri nchi za Afrika kuungana pamoja kuhakikisha vita vinavyoendelea katika mji wa Goma nchini DR Congo vinaisha kwa haraka.
![](https://www.lajiji.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001195045.jpg)
Aidha, asasi hizo leo Februari, 7 2025 zimetangaza kuunga mkono jitihada zinachukuliwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini kwa Afrika (SADC), kuleta amani na utulivu nchini DR Congo.
Mji wa Goma umeingia kwenye mapigano kati ya Waasi wa Kundi la M23 ambapo inadaiwa zaidi ya watu 850 wameuwawa kwa kipindi cha wiki moja.
Asasi hizo zimetoa ushauri na uungaji mkono juhudi za viongozi wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo wamekutana kuzungumzia hali ya jijini Goma nchini DR Congo.
![](https://www.lajiji.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001195044.jpg)
Kwa upande wake Kennedy Walusala kutoka Asasi ya Kiraia nchini Kenya, alisema mauji ya watu 850 sio ya kufumbiwa macho hivyo wameamua kukutana kuzungumza an kujadiliana namna ambayo itawezesha DR Congo itapata amani.
“Sisi kama asasi za kiraia tunapambana kutafuta amani ili kuweza kuwafanya wananchi waishi kwa amani.
Lakini pia tumeamua kukutana hapa Dar es Salaam kabla ya viongozi hawajakutana ili kuwaunga mkono.
Walusala amesema katika kuhakikisha amani inapatikana DR Congo wanaomba vyombo vya habari na waandishi kufanya kazi kizalendo ili kuepuka utoaji wa habari zenye utata.
![](https://www.lajiji.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001195043.jpg)
“Kinachoendelea DR Congo hakipaswi kuonekana kama matangazo bali misingi ya utu inapaswa kuungwa mkono kila siku.
Mwanasheria wa Kamati Amani na Ulinzi nchini DR Congo, Eloi Bugoye alisema iwapo nchi za Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla wakiamua kumaliza kinachoendelea Goma inawezekana bila shida yoyote.
Amesema kinachoendelea DR Congo kikiachwa matokeo yake yatakuwa mabaya siku zijazo, hivyo ni vema kila nchi kushiriki kikamilifu kumaliza tatizo hilo.
Bugoye amesema hatuwezi kuendelea kusema mabaya mazuri na mazuri mabaya, bali ni wakati wa kushikamana kwa kufanyia kazi maazimio ambayo yanatolewa mara kwa mara.
“Huwa tunajiuliza nani anafaidika na watu kuuwawa, lakini ukiangalia sababu kubwa ni watu kukosa utu na kuamua kuuwa watu bila kosa lolote, hivyo sisi asasi za kiraia tupo tayari kushirikiana na kila mdau kuhakikisha vita inakwisha,” amesema.
Amesema hali ni mbaya huko Goma, hivyo ni wakati muafaka kwa kila mpenda haki kuungana na asasi za kiraia kukemea mauaji hayo, kwani wao hawana silaha za moto za kukabiliana na waasisi.
“Napenda kuwaomba watu wote wa nchi za Maziwa Makuu tuungane na viongozi wetu kuhakikisha tunamaliza mgogoro unaoendelea Goma,” amesema.
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia za Nchi za Maziwa Makuu, Joseph Butiku amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kukubali kuwapokea viongozi wa EAC na SADC ili kutafuta suluhu ya mgogoro nchini DR Congo.
Butiku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF ) amesema maamuzi yatakayotolewa na viongozi watayaunga mkono kwa sababu wanaamini yatamaliza vita hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema DR Congo ni nchi kubwa na ina utajiri wa kutosha, ili amani na usalama ndio vitafanya wananchi wake kunufaika na rasilimali zilizopo.
“DR Congo ni nchi ambayo inapakana na nchi nyingi, matatizo ya vita yamesababisha wengi kuikimbia nchi yao na tatizo hilo ni dharura ndio maana tumekutana hapa kuwaonesha viongozi wetu kwamba tupo nao katika kutafuta suluhu,”amesema.
Siku nne zilizopita nilipigiwa simu na viongozi hawa wa Kamati ya Amani na Usalama ya DR Congo wakiomba tukutane tuzungumze na sisi tumeona ni vema tuzungumze kwa maslahi ya nchi zetu kutafuta suluhu ya jambo hilo vita.
“Niwapongeze viongozi wetu kwa kuona uzito wa jambo hili na tunampongeza Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuita wenzake nchini, aliombwa lakini amekubali kuzungumza tatizo hili, matumaini yetu watapata suluhu ya DRC iwe na amani,” amesema.