Home AFYA MOI YAANZA RASMI KUFANYA UPASUAJI WA UTI WA MGONGO KWA NJIA YA...

MOI YAANZA RASMI KUFANYA UPASUAJI WA UTI WA MGONGO KWA NJIA YA MATUNDU

Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza rasmi kutoa huduma mpya za upasuaji uti wa mgongo kwa kutumia matundu (Spine Endoscope).

Pia amesema kuanza kutolewa kwa huduma hiyo kutasaidia ufanisi wa upasuaji huo na kuwezesha wagonjwa kukaa siku cheche wodini.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amebainisha hayo leo Februari, 5, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya kibingwa ya uti wa mgongo kwa njia ya matundu ambapo wagonjwa 12 watafanyiwa upasuaji.

Ameeleza kuwa MOI inakuwa taasisi ya kwanza nchini kutoa huduma hizo baada ya kupokea mashine ya kisasa (Endoscope tower) ya kufanyia upasuaji huo yenye thamani ya shilingim milioni 500 kutoka kampuni ya Joimax ya nchini Ujerumani na kuifanya Taasisi ya MOI kuwa kinara katika utoaji wa huduma za upasuaji wa uti wa mgongo kwa matundu katika ukanda wa Afrika mashariki , Kati na Kusini na kuchagiza dhana ya Tiba Utalii.

“MOI imekuwa Taasisi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwa na kifaa hiki cha kisasa cha upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu…ufanisi wa upasuaji utaongezeka na wagonjwa watapona kwa haraka na kupunguza muda wa kukaa wodini,” amesema Dk. Ulusubisya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo na Uti wa mgongo, Dk. Lemeri Mchome amesema huduma hiyo itasaidia wagonjwa kupata nafuu kwa haraka kutokana na kupata jeraha ndogo wakati wa upasuaji.

“Awali Taasisi ya MOI ilikuwa ikifanya upasuaji kwa kwa kufungua eneo kubwa hivyo kumlazimu mgonjwa kukaa muda mwingi wodini akiuguza jeraha na kumuacha na kovu kubwa… mgonjwa alikuwa analazwa siku tano au zaidi baada ya upasuaji kutokana na ukubwa wa jeraha, pia maumivu kwa mgonjwa yalikuwa makali, lakini kwa kutumia mashine hii changamoto hizo zote zitakuwa zimeisha,” amesema Dk.Mchome.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Weill Cornel cha nchini Marekani, Dk. Osama Nazar Kashlan ameipongeza Taaisis ya MOI kwa kuwa tayari kuwekeza katika ujuzi wa watumishi wake na kuahidi kuendelea kuwajengea uwezo katika huduma za kibingwa na kibobezi ili waendane na mabadiliko ya teknolojia duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here