Home MICHEZO TANZANIA IMEJIPANGA MAANDALIZI CHAN NA AFCON – MAJALIWA.

TANZANIA IMEJIPANGA MAANDALIZI CHAN NA AFCON – MAJALIWA.

Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga vyema kukamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu kwa ajili ya Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Africa CHAN na AFCON.

Ameyasema hayo leo Jumamosi Februari Mosi, 2025 aliposhiriki katika Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

“Tanzania imejipanga vizuri, kuhakikisha kuwa michuano hii inafanyika hapa Nchini, Serikali inawajibika kuhakikisha inaandaa viwanja na miundombinu mingine,”amesema

Amesema kuwa tayari ukaguzi wa baadhi ya viwanja umefanyika na vimeonekana kukidhi vigezo.

“Viwanja vilivyokaguliwa vipo Tanzania bara na Visiwani, na kazi bado inaendelea, lengo ni kuhakikisha michuano hii inafanyika kwa ufanisi,”amesema.

Majaliwa amesema ni vyema sasa Watanzania wakajipanga kutumia fursa zitakazo jitokeza kutokana na kuwepo kwa michuano hiyo hapa Nchini.

“Hii ni fursa kwetu Watanzania, lazima tujipange kutumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza, ili tuweze kunufaika,”amesema.

Aidha,Waziri Mkuu amempongeza Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson kwa kuandaa Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza ambalo limewakutanisha wabunge na wanamichezo mbalimbali wa Mkoani Dodoma.

“Tamasha hili limekuwa na mafanikio makubwa, limetupa nafasi wabunge kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuimarisha afya zetu,”amesema.

Amesema ni vyema Watanzania wakaendelea na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here