Dar es Salaam
UONGOZI wa mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kufanya mazungumzo na Shirika la Reli nchini (TRC) ili kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wakua kujenga reli yakusafirisha abiria ndani ya mkoa huo.
Akizungumza leo Januari, 30 jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mrejesho wa mkutano wa nishati Afrika uliofanyika siku mbili,Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema lengo la treni hiyo ni kupunguza adha ya usafiri mkoa huo.
“Fedha tunazozikusanya kwa mkoa wa Dar es Salaam zinafika si chini ya Shilingi bilioni 300 Jumanne ijayo tutakaa pamoja na Mkurugenzi wa TRC kuangalia namna yakujenga reli ya kawaida inayobeba abiria ambayo itakuwa ni ubia TRC na watu binafsi na halmashauri,”amesema Chalamila.
Amesema ujenzi wa reli hiyo na njia ambayo itajengwa utajulikana baada ya watalaam kufanya upembuzi yakinifu na kuona sehemu gani inapaswa kujengwa.
Mbali na hilo Chalamila pia ametangazwa kuanza kwa utaratibu wa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa masaa 24 kuanzia Februari 22 mwaka huu.
“Katika kuelekea kufungua zaidi mkoa wa Dar es Salaam mimi na wenzangu tumekubaliana Dar es Salaam ianze kufanya biashara saa 24,kwa maana hiyo Februari 22 ndio itakuwa siku rasmi yakufungua.
Awali tulipanga Februari,8 tumepeleka mpaka Febriari 22 kwa sababu kuna baadhi ya maeneo hatujafika kuyaweka taa na maboresho mengine madogo madogo,”amesema Chalamila.
Amesema kwakuanza kwa utaratibu huo siku ya kwanza ya uzinduzi wafanyabiashara watafanya biashara masaa 24 kuanzia eneo la viunga vya kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa hadi Kariakoo.
Mbali na hilo ofisi ya mkuu ya mkoa wamekubaliana mambo mbalimbali kutokana na mji huo kukua kwa kasi ikiwemo masuala kuboresha majengo chakavu.
“Kutokana na mji wetu kukua kwa kasi tumekubaliana yafuatayo kuunda kamati maalum kuangalia majengo chakavu na yaliyochoka,baada ya hapo kamati itashirikiana na wenye majengo kutafuta wafadhili ili kufanya maboresho ya majengo hayo,”amesema.
Amesema kamati pia itafanya uuishaji wa sheria ya kusimamia usafi na kuweka vifaa vya kuhifadhia taka ili mji uwe safi na salama.
“Tutaendelea kushirikiana na wananchi kuhusu ufanyaji wa usafi ambapo itakuwa kila Jumamosi ya wiki itakuwa inafahamika kama siku ya usafi kabambe,”alisema Chalamila.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wafanyabiashara wa soko dogo la Kariakoo,Hawa Ghasia amesema uongozi wa soko dogo la Kariakoo leo unatarajia kupandisha majina ya wafanyabiashara zaidi ya 800 kati ya 1,520 ambao awali walikuwa katika eneo hilo.
Amesema soko hilo ambalo limeshakamilika kwa asilimia 98 limekarabatiwa kwa gharama ya Sh Bilioni 28 baada ya kuungua Novemba mwaka jana wafanyabiashara wake wataanza kupewa utaratibu wakupata vizimba hivyo leo.
“Tunakusudia kesho (leo) kupandisha majina ya wafanyabishara waliokuwepo awali kabla ya soko alijaungua baada ya kumalizana na waliokuwepo tutatangaza utaratibu kwa wafanyabiaashara wapya ambao watatuma maombi yao kupitia mfumo wa Tausi,”amesema Ghasia.
Amesema majina ya wafanyabiashara watakaopandishwa katika mtandao huo ni zaidi ya 800 kati ya 1520 waliokuwepo huku wafanyabiashara 366 hawataweza kuingia katika mfumo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kudaiwa kwa muda mrefu.
“Wafanyabiashara ambao walikuwa wanadaiwa wanatakiwa kulipa kabisa ili kuepuka usumbumbufu wakati wa kukabidhiwa maeneo yao,”amrsema Ghasia.
Amesema pamoja kutokea ajali ya moto kuna watu walikuwa wanalipa madeni yao tutaangalia madeni kwa kesi na kesi lakini waliokuwa na madeni yao sugu lazima walipe.