Home KITAIFA DK. BITEKO AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI KWA RADI GEITA

DK. BITEKO AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI KWA RADI GEITA

๐Ÿ“Œ Rais Samia atuma salamu za pole, agharamia misiba na mazishi

๐Ÿ“Œ Mkuu wa Wilaya Bukombe aishukuru Idara ya Afya kwa juhudi za maokozi

๐Ÿ“Œ Viongozi wa dini wahimiza uvumilivu na uhimilivu kipindi cha majonzi

Geita

LEO Januari 30, 2025 mkoani Geita, maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga miili ya wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe waliofariki kwa kupigwa na radi mnamo tarehe 27 januari, 2025.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dk. Doto Biteko ameongoza shughuli za kuaga na kukabidhi ubani kwa wafiwa huku akiwataka kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki cha majonzi.

Ametoa pole kwa wazazi, walezi ndugu wa watoto pamoja na wanafunzi wa Businda kwa kuondokewa na wapendwa wao na wanajamii wa Businda Sekondari kwa jitihada na utoaji wa huduma wakati wa tukio hilo.

โ€œ Imeandikwa kwamba shukuruni Mungu kwa kila jambo, Mungu ametukutanisha leo katika hali ya majonzi. Tukio hili litukumbushe kutenda mema wakati wote na tuamini kwamba Mungu ndiye mwenye uweza. Kipekee ningetamani kuwataja Madaktari wote kwa majina kutokana na msaada mkubwa walioutoa lakini itoshe kusema asante
kwa kazi kubwa mliyoifanyaโ€ amesema Dk. Biteko.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito amekuwa akifuatilia kwa karibu na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuzifariji familia za wafiwa, wana Bukombe na Taifa kufuatia kuondokewa na vijana waliokuwa katika safari ya kutafuta elimu.

โ€œRais Samia amegharamia msiba pamoja na kutoa ubani kwa kila familia za wafiwa pamoja na kugharamia usafirishaji wa miili ya wanafunzi wawili kwenda Chato, Geita na Karatu mkoani Arusha kwa mazishi,”amesema.

Viongozi mbalimbali wa dini wamewapa faraja wafiwa na kusema msiba haujawahi kuzoeleka lakini kwa mapenzi ya Mungu atakuwa mfariji wao.

Viongozi hao wamewataka wanadamu kujipanga wakati wote kwa kuwa hawajui ni wakati gani utafikwa na umauti kutokana na fumbo aliloliweka Mwenyezi Mungu.

Aidha, wamemwomba Mungu awape uvumilivu viongozi katika kipindi hiki cha majonzi.

Wanafunzi hao saba waliokuwa wakisoma kidato cha tatu walikuwa na umri kati ya miaka 16 na 18, walikutwa na umauti kwa kupigwa na radi wakati wakiendelea na masomo darasani.

Waliofariki ni Erick Emmanuel Akonaay (17), Nikas Paul Tompoli (18) Gabriel Daud Makoye (17), Doto Marco Masasi (18), Asteria Reonard Mkina (16), Peter Nkinga Manyanda (17) na Erick Martine Bugalama (16).

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Theodora James Mushi amesema wanafunzi hao walipatwa na umauti wakiwa katika harakati za kusaka elimu.

Wanafunzi wanne kati yao walifariki papo hapo na wengine watatu walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali na vituo mbalimbali vya Afya.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskazi Mragili ameishukuru Idara ya afya kwa utayari na uharaka wa utoaji huduma kwa wanafunzi wote 138 ambapo wanafunzi 89 waliathirika moja kwa moja na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani. Majeruhi wote wameruhusiwa na wale waliopata majeraha wanaendelea kutibiwa wakitokea nyumbani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here