RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania ni moja Kati ya nchi 12 zitakazozindua Mpango Mahususi wa kitaifa kuhusu nishati na kupitia mpango huo wanatarajia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.
Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 28,2025 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika 2025 (Mission 300) unaendelea kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), mkutano huo unalenga kuwapelekea umeme waafrika milioni 300 katika nchi za Afrika
Amesema ili kufanikisha adhma hiyo ndani ya muda wa miaka mitano ijayo nchi itahitaji uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 13 ambapo Dola Bilioni tano zitapatikana kutoka sekta binafsi za hapa nchini.
Rais Dk. Samia amesema kupitia mpango huo wamepanga kutekeleza mambo makubwa manne ambayo ni kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na nishati mchanganyiko.
Amesema hadi sasa Tanzania una uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 3,431 ambapo asilimia 58 ya hizo zinatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 inatokana na gesi huku asilimia sana inatokana na vyanzo vingine.
Amesema shabaha ya nchi ni kuongeza megawati 2463 za nishati ya jua, gesi asilia, upepo, joto ardhi na vyanzo vingine ifikapo 2030.
“Jambo la Pili kijographia Tanzania ni kiungo muhimu katika kuunganisha mtandao wa umeme kwa nchi za mashariki na Kusini kwa Afrika na hivyo kuwezesha biashara ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Misri, tayari tumekwisha unganisha miundombinu ya umeme na nchi za Burudi, Kenya na Rwanda na sasa tunaendelea kuunganisha miundombinu ya umeme na nchi ya Zambia na Uganda,” amesema Rais Dk.Samia.
Amesema kuwepo kwa miundombinu hiyo itawezesha biashara ya nishati Kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema Tanzania inayonafasi ya kuuza umeme ikizingatiwa kuwa hadi Novemba mwaka 2024 mahitaji ya umeme nchini yalikuwa megawati 1,888 wakati uzalishaji ukiwa megawati 3,431.
Rais Dk.Samia amesema Tanzania inahitaji kufikisha umeme kwenye vitongoji baada ya kufanikiwa kupeleka nishati hiyo katika vijiji vyote vilivyopo nchini.
“Mwelekeo wetu ni kuvifikia vitongoji 64,359 lakini hadi sasa tumeshavifikia vitongoji 32,827 na kazi inaendelea katika vitongoji 20,000 na kupitia mpango huu tutaweza kuvifikia vitongoji 11,532 vilivyobakia,” amesema.
Pia amesema mpango huu utasaidia usambazaji wa Nishati safi ya kupikia huku inakadiliwa watu 950 barani Afrika wanakosa nishati hiyo hali ambayo inalighalimu bara hilo na kwamba inahusishwa na kuongezeka kwa umasikini, vitishio vya kiafya, uharibifu wa mazingira, kuongezeka uzalishaji wa kaboni, kupotea kwa baonuai na kukosekana kwa usawa wa kijinsia.
“Nchini Tanzania utegemezi wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni zaidi ya asilimia 90, hatuwezi kupuuza madhara na gharama kubwa ya kutumia kuni na mkaa hasa kwa afya na ustawi wa wanawake na wasichana.
“Katika kukabiliana na hilo Tanzania tumeweka mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha cha matumizi ya nishati safi ya kupikia toka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo 2034, mpango mahususi tunaozindua leo utasogeza karibu kufikia lengo hilo,” ameeleza.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinumwi Adesina amesema upatikanaji wa umeme ni jambo la muhimu katika bara la Afrika na ukosefu wa nishati hiyo unadhoofisha uchumi wa nchi moja moja.
Amesema asilimia kubwa ya waafrika kwa sasa hawana umeme na ndio maana wameleta agenda hiyo ya Mission 300 ili kuhakikisha watu wanafikiwa na huduma hiyo ili kukuza uchumi wa nchi za Afrika.
Amesema hawataweza kufanikiwa jambo hilo kama hawataweza kufanyakazi pamoja sekta binafsi na ndio maana wamefika katika mkutano huo kukubaliana ni kwa namna gani watatekeleza jambo hilo la kuwafikishia umeme watu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira.
“Benki ya Dunia (WB) na AfDB tunalenga kutoa Dola za Marekani Bilioni 40 kama kianzio cha kuhakiksha tunafanikiwa katika Mission 300,” amesema.
Naye Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga amesema mikakati yao ni kujielekeza katika kubadili maisha ya Afrika na Mpango wao ni kuhakikisha watu milioni 300 Afrika wanapata umeme ili wawe kichocheo cha upatikanaji wa ajira.
“Hata hivyo hatuwezi kufanikiwa kwa kumuangalia mtu mmoja, nchi zinatakiwa kushirikiana na kuandaa mipango ambayo itajielekeza kupata umeme hasa wa gharama nafuu,” amesema Banga.