*Lengo ni kuwezesha utoaji wa utabiri na tahadhari za hali mbaya ya hewa
Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ikiwemo upande wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kujenga uwezo wa wafanyakazi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo Januari 21, 2025 alipozindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF) – Project” katika Ukumbi wa Hotel ya Midland Inn View, Dodoma.
Majaliwa amesema lengo la Serikali la kuendelea kufanya maboresho hayo ni kuwezesha utoaji wa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
Amesema miongoni mwa uwekezaji huo ni ununuzi wa rada saba za hali ya hewa, upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa kwa kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Minamata.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ya Tanzania katika kuunga mkono utekelezaji wa mradi wa SOFF imetenga fedha za kununua Vituo 11 vya Hali ya Hewa. Vituo hivyo vinavyojiendesha vyenyewe vitachangia data katika Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi.
Pia, amesema Serikali inaunga mkono kwa kutoa mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni nne ambazo ni thamani ya mchango kwa njia ya huduma zisizo za kifedha (In-Kind contribution). “Jitihada zote hizo, zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa.”
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mradi wa SOFF “SOFF – Investment Phase Project”, Majaliwa amesema mradi huo una umuhimu mkubwa siyo tu kwa kukidhi mahitaji ya data za hali ya hewa na tabianchi kwa ajili ya utabiri wa hali ya hewa duniani, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na ubadilishanaji data za hali ya hewa kimataifa, hivyo kuimarisha huduma za hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
“Mafanikio katika utekelezaji wa SOFF yatachangia sana kuimarisha ustahimilivu wa matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maendeleo endelevu nchini,”amesema.
Amesema kuwa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea unategemea sana sekta zinazohusiana moja kwa moja na hali ya hewa, ambazo ni kilimo, lakini pia, ufugaji, nishati, maji, afya, madini na usafirishaji.