Home KITAIFA DK. JAKAYA KIKWETE ATOA USHAURI WA KIBUNIFU WAGOMBEA URAIS CCM

DK. JAKAYA KIKWETE ATOA USHAURI WA KIBUNIFU WAGOMBEA URAIS CCM

Dodoma

RAIS Mstaafu Dk.Jakaya Mrisho Kikwete ameonyesha hekima ya hali ya juu na uzoefu wake katika siasa kwa kutoa ushauri thabiti unaolenga kuimarisha umoja na uwazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo Januari, 19 2025 katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM mjini Dodoma, ulioongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Kikwete amesisitiza umuhimu wa kufuata utaratibu rasmi wa chama kwa kupitisha azimio la kuidhinisha majina ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kama wagombea wa urais wa mwaka 2025.

Katika hotuba yake, Kikwete amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao na ameeleza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao hauna shaka kutokana na mafanikio yaliyopatikana.

“Kama tumekubaliana katika mkutano huu, basi Rais Samia na Rais Mwinyi wanaelekea kushinda tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Lakini ni muhimu tupitishe azimio rasmi ili kuhakikisha tunazingatia taratibu za chama na kutoa ujumbe wa mshikamano kwa wanachama wote,” amesema Kikwete.

Kwa kuhitimisha, Kikwete amewatia hamasa wajumbe kwa kuanzisha wimbo wa kuonyesha imani kwa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi, ambao ulizua shangwe kubwa katika ukumbi wa mkutano.

Hatua hii ya Rais Mstaafu Kikwete imeonyesha uzalendo na umakini wake katika kulinda mshikamano wa CCM, huku ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na taratibu ndani ya chama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here