Handeni
WATU 11 wamefariki dunia wa Kijiji cha Chang’ombe kilichopo Kata ya Segera wilayani Handeni Mkoani Tanga baada ya kugongwa na lori lililokuwa limebeba saruji baada ya kupoteza uelekeo wakati walipojitokeza barabarani walipokuwa wakishanga ajali ya gari dogo aina ya tata .
Watu hao walijitokeza barabarani ili kuweza kutoa msaada kufuatia ajali ya barabarani ya gari dogo aina ya Tata ndipo walipokumbana na ajali hiyo iliyopelekea kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian lori hilo liliwagonga watu hao usiku wa kuamkia Januari 14,2025 na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi.
Lori hilo lenye namba za usajili T.680 BQW likiwa linatokea Tanga lilifeli breki na kuwagonga watu waliokuwepo pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo vya watu 11 papo hapo na kujeruhi wengine 11.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Korogwe Magunga na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huyo ametoa pole kwa familia za marehemu na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi wote .
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali nzuri ya kiufundi ili kuepusha ajali za namna hiyo.