Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amehimiza umuhimu wa majadiliano ya pamoja badala ya ukosoaji ili kujenga uelewa wa pamoja utakaofanikisha upatikanaji wa dira ya maendeleo 2050 itokanayo na maoni ya wananchi na wadau mbalimbali.
Kauli hiyo ametoa leo Januari, 10 2025 na Naibu Waziri Nyongo wakati akifungua Mkutano wa Asasi za Kirai (AZAKI) waliokutana kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 amesema kazi iliyofanywa na Asasi hizo za kirai imeingia kwenye historia ya Taifa kwaajili ya kizazi kijacho.
Amesema Serikali imejiandaa vya kutosha kusikiliza kila maoni ya wadau na wananchi jambo hilo ni muhimu zaidi ili kuhakikisha kuwa dira 2050 inakuwa halisi na inayotokana na maoni ya wananchi.
“Wakati nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii nilikutana mara kwa mara na Asasi hizi za kiraia usipowaelewa dhamira yao ya kukumbusha baadhi ya mambo, huenda ukafikiri kuwa wansikosoa serikali kila wakati jambo ambalo sio la kweli,” amesema Nyongo.
Amesema wamepokea maoni ya makundi mbalimbali ikiwemo wanasiasa, wafanyabiashara, taasisi za kibenki makundi maalum walemavu, vijana na wengineo.
Ameongeza kuwa kifuatacho ni mikakati Tume itakaa kuandaa dira ya maendeleo 2050 na wataalamu watazingatia maoni kwenye kilimo, elimu, afya na sekta zote nini kifanyike ili waanze kutekeleza dira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge amebainisha kuwa kukuza uchumi shindani ndani ya mikoa ni njia muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu, akitolea mfano wa nchi ya Kenya ambako kaunti zinashindana kwa vigezo vya kuzalisha ajira na kujumuisha makundi ya pembezoni.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuwajumuisha wadau wa kiraia katika uandishi wa Dira ya Maendeleo ya taifa ya mwaka 2050.
Kwa upande wake Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Lucas Kifyasi,ameongeza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utahitaji kipaumbele katika elimu, hasa kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda yanayotarajiwa kuimarika miaka 25 ijayo.
Amesisitiza kuwa elimu na teknolojia ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu katika nchi.