Dar es Salaam
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amesema ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha kushindilia gesi asilia (CNG) kilichopo Ubungo, ambapo ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho mapema mwaka huu kutawawezesha Watanzania, hususan wanaotumia gesi asilia kwenye magari, kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Hayo ameyabainisha leo Januari, 9 jijini Dar es Salaam Dk. Biteko wakati alipotembelea na kukagua kituo hicho kinachojengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuelezea kuwa kuanzia Februari, 3 Mwaka huu, kituo hicho kitaanza kutoa huduma ya kujaza gesi asilia kwenye magari.
Amesema serikali imeelekeza kujengwa kwa vituo vingine vya gesi asilia, ambapo vituo saba vya ziada vinajengwa na sekta binafsi katika Mkoa wa Dar es Salaam huku wizara ya Nishati imepanga kuanzisha vituo vinavyotembea vya kujaza gesi asilia katika mikoa ya Morogoro kituo moja na Dodoma viwili.
“Vituo hivi vinajengwa na kampuni tanzu ya TPDC na leo tumetembela kituo hichi kuangalia maendeleo ya ujenzi nimeridhishwa na kasi ya ujenzi huu unavyoendelea. Mkandarasi ametuhakikishia itakapofika Februari 03, 2025 kwa mara ya kwanza magari yatakuwa yanakuja kujaza gesi hapa,” amesema Dk. Biteko.
Amesema malengo ni kuondoa foleni ambazo zinajitokeza katika vituo vya kujazia gesi katika magari, Pikipiki na Bajaji.
Amesema mwitikio wa Watanzania kuhama kwenye matumizi ya mafuta kwenda kwenye nishati safi umekuwa mkubwa sana ndio maana watu wanaotumia vyombo vya usafirishaji wanatumia gesi asilia
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema wamekubaliana na Shirika la Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuleta mabasi yanayotumia gesi asilia hatua inalenga kuhamasisha Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kimetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo,Profesa William Anangisye amefafanua kuwa mradi huo utatoa fursa kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi kutumia kituo hicho kama sehemu ya mafunzo ya vitendo.
Pia amesema kuwa watahakikisha kituo hicho kipo salama muda wote kutokana na kuwa katika eneo hilo. Na ajira nyingi zitakazopatikana zitasaidia vijana wa kitanzania.