Home AFYA MOI YAWAOMBA WATANZANIA KUJITOKEZA KUCHANGIA DAMU

MOI YAWAOMBA WATANZANIA KUJITOKEZA KUCHANGIA DAMU

Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewaomba Watanzania kujitokeza katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi wanaohitaji huduma hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Januari, 08 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Cresencia Mwibari wakati akijibu hoja na maoni ya wagonjwa na ndugu wa wagonjwa eneo la kusubiria huduma lililopo katika taasisi hiyo.

Cresencia amesema kuwa uhitaji wa damu ni mkubwa, ambapo kwa siku taasisi hiyo hutumia wastani wa chupa 20 hadi 30 kwa ajili ya majeruhi wa ajali mbalimbali zikiwemo za barabarani.

“Napenda kutoa rai kwa Watanzania wenzangu kuja kuchangia damu katika Taasisi ya MOI, hii ni hospitali ambayo inadili na majeruhi wa ajali mbalimbali, wagonjwa wanakuja wakiwa wamepata majeraha wamemwaga damu, kwahiyo asilimia kubwa wagonjwa huongezewa damu.

Taaasisi yetu (MOI) hutumia chupa 20 hadi 30 za damu kwa siku, tukipata watu (watanzania) watakaokuja kuchangia damu itasaidia na damu itapatikana kwa wingi,”amesema Cresencia.

Pia amewakumbusha wachangiaji wa damu salama wa muda mrefu wanaofika katika taasisi hiyo kupatiwa huduma za matibabu kwenda na kadi zao za uchangiaji damu na kuziwasilisha katika idara ya maabara ya MOI kwa ajili ya kufanyia uhakiki na uthibitisho.

Kwa upande wake, Philimon Ndaki amewapongeza watumishi wa MOI kwa kumpatia huduma za kuridhisha za matibabu, kwani alifanyiwa upasuaji miaka minne iliyopita na sasa anaendelea vizuri na kuhudhuria kliniki kila baada ya miezi sita katika taasisi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here