Dar es Salaam
KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanya tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini na kuamua kuendelea kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia sita katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Akizungumza leo Januari, 8 2025 jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema uamuzi huo umetokana na kikao chake cha kila robo mwaka kilichofanyika Januari, 07 mwaka huu.
Amesema kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, Kamati ilibaini kuwa ripoti zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, zinaonesha ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa imara katika mwaka 2024.
Ameeleza kuwa katika robo ya nne ya mwaka 2024, Kamati ilibaini kwamba mazingira ya uchumi duniani yaliimarika kwa kiwango kikubwa, ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka, mfumuko wa bei uliendelea kupungua katika nchi nyingi, na mazingira ya upatikanaji wa fedha kwa riba nafuu katika masoko yaliimarika.
“Uamuzi huo wa kamati wa kutobadili Riba ya Benki Kuu unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia tano na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takriban asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
“Aidha, uamuzi huo unalenga kuwa na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni kuendelea kuwa na mfumuko wa bei mdogo. Utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni utachangia jitihada za kuwafanya wananchi kutofanya miamala yao kwa kutumia fedha za kigeni nchini,”amesema.
Amesema bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi, zilipungua. Hali hii ilichangia kuimarika kwa uchumi nchuni hivyo mazingira hayo mazuri ya kiuchumi yanatarajiwa kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na ongezeko la mahitaji ya walaji, sera wezeshi za bajeti na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha kwa riba nafuu.
Amesema matarajio hayo yanaweza kuathiriwa endapo migogoro ya kisiasa duniani na mivutano ya kibiashara itaongezeka.
“Kamati iliridhishwa na mwenendo wa uchumi wa hapa nchini kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti na maboresho ya kukuza uchumi, kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani kumechangia kuendelea kuimarika kwa uchumi,”amesema.
Amesema kuimarika kwa uchumi pia kulithibitishwa katika tathmini iliyofanywa na Kampuni ya Fitch Ratings Desemba mwaka jana, ambapo uchumi umendelea kubakia katika alama ya B+ yenye matarajio ya kuendelea kuimarika.
Vilevile, IMF iliridhika na mwenendo wa uchumi katika tathmini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) na Resilience and Sustainability Trust (RST).
MWENENDO WA UCHUMI
Akizungumzia mwenendo wa uchumi Gavana Tutuba amesema uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuwa imara kwa mwaka jana.
” Uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024, na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya nne ya mwaka jana, kwa kuzingatia mwenendo huo, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa sawia na maoteo ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka jana. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na ongezeko la shughuli za kilimo, usafirishaji, ujenzi, na biashara.
“Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 katika robo ya ya kwanza na asilimia 7.2 katika robo ya pili ya mwaka 2024, na unakadiriwa kukua kwa viwango hivyo kwa robo mbili zinazofuata, hivyo kufikia maoteo ya ukuaji wa asilimia 7.2 kwa mwaka 2024, ukichangiwa na shughuli za utalii, ujenzi, na viwanda, “amesema.
Amesema kwa mwaka huu, ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar unatarajiwa kuendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha, kwa takriban asilimia sita na asilimia 6.8 mtawalia.
Aneongeza kuwa ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.
Amesema mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu katika kipindi chote cha mwaka 2024, ukiwa chini ya lengo la asilimia tano kwa Tanzania Bara na kukaribia lengo hilo kwa upande wa Zanzibar. Katika robo ya nne ya mwaka 2024, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia tatu kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi.
Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.5, Novemba 2024 hivyo mfumuko huo unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia nne.
Amesema hali hii inatokana na kuendelea kuwepo kwa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi.
Pia ukuaji wa ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9, mtawalia. Katika robo ya nne ya mwaka 2024, ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 14.8 kwa mwaka ikilinganishwa na asilimia 13.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 16.8 ikilinganishwa na asilimia 17.8.
Mwenendo huu unatokana na ongezeko la mahitaji ya mikopo mipya kufuatia kuimarika kwa uchumi wa dunia na hapa nchini, pamoja na kupungua kwa vihatarishi katika ukopeshaji kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu kufikia asilimia 3.6 Novemba, mwaka jana kutoka asilimia 4.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Alisema ukwasi wa fedha za kigeni uliongezeka kwa kiwango kikubwa katika robo ya nne ya mwaka 2024. Hali hiyo inatokana na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha duniani kutokana na kupungua kwa riba katika nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni nchini kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku.
Pia utekelezaji wa sera ya fedha uliolenga kupunguza athari za kushuka kwa thamani ya shilingi kwenye mfumuko wa beiulichangia kuiimarisha shilingi.
KUIMARIKA KWA SHILINGI
“Kutokana na kuimarika kwa ukwasi wa fedha za kigeni nchini, shilingi iliimarika dhidi ya fedha za kigeni, soko la fedha za kigeni lisilo rasmi lilitoweka, na matarajio kuwa thamani ya shilingi itaendelea kushuka yalififia. Hali hiyo ilikuwa na manufaa ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo, na kupunguza gharama ya kulipa madeni nje ya nchi.
“Thamani ya shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, kutokana na kuwepo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024, utekelezaji wa sera ya fedha kutokana, uamuzi wa kubakiza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia sita na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.
Vilevile, utachangiwa na Benki Kuu kuendelea kusimamia utekelezaji wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu kinachohimiza matumizi ya shilingi katika kufanya miamala hapa nchini kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima, “amesema.
FEDHA ZA KIGENI
Gavana Tutuba amesema Benki Kuu inatarajia kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni na kuongeza fedha za kigeni pale itapohitajika.
“Akiba iliyopo sasa ni zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.5, kiwango ambacho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.7.
“Akiba hiyo inatarajiwa kubaki katika kiwango hicho katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na juhudi zinazofanywa na Benki kuu katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ikiwemo kununua dhahabu hapa nchini,” amesema.
MAKUSANYO YA MAPATO NA DENI LA TAIFA
Gavana Tutuba amesema utekelezaji wa sera ya bajeti ulikuwa wa kuridhisha, ambapo makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi yalivuka malengo, kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, maboresho katika usimamizi wa kodi na utayari wa wananchi kulipa kodi.
Aidha, matumizi ya Serikali yaliendelea kufanyika kuendana na rasilimali zilizopo.
“Deni la Taifa liliendelea kuwa himilivu, ambapo kwa mwaka 2023/2024 lilikuwa takriban asilimia 41.1 ya Pato la Taifa (GDP) kwa thamani halisi ya sasa (NPV). Kiwango hiki kilikua chini ya ukomo wa uhimilivu wa nchi na kigezo cha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha asilimia 55 na asilimia 50, mtawalia.
” Kwa kuzingatia thamani ya bei za sasa, deni la Taifa lilikuwa asilimia 46.1 ya Pato la Taifa, chini ya kigezo cha mtangamano kwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) cha ukomo wa asilimia 60, ” amesema.
MAUZO YA NJE YA NCHI
Anesema sekta ya nje iliendelea kumarika zaidi katika mwaka 2024. Nakisi ya urari wa malipo ya nje ilipungua kufikia asilimia 2.7 ya Pato la Taifa, ikiwa ni nakisi ya chini kabisa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, na ikilingashwa na asilimia 3.7 mwaka 2023.
Amesema hali hiyo ilitokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
“Mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yanakadiriwa kufikia takriban asilimia 20 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 18 katika mwaka uliotangulia, kutokana na ongezeko la shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku nje ya nchi. Uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje ya nchi ulikuwa asilimia 21 ya Pato la Taifa ukilinganisha na asilimia 20.3 mwaka 2023, ” amesema.
Pia, katika robo ya nne ya mwaka 2024, urari wa malipo ya kawaida ulikadiriwa kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 643.4, ikiwa ni takriban nusu ya nakisi iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kwa upande wa Zanzibar, urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 124.5, ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 136.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, kutokana na ongezeko la uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
“Sekta ya nje inatarajiwa kuendelea kuimarika mwaka 2025, ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida kwa Tanzania Bara unatarajiwa kupungua hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa.
“Benki Kuu itaendelea kuhakikisha uwepo wa ukwasi unaoendana na mahitaji ya uchumi, kufikia malengo ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo na kuchagiza ukuaji wa shughuli za uchumi na kufikia malengo haya, Benki Kuu itaendelea kufuatilia mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika,” amesema.
Amesema kamati itakutana tena wiki ya kwanza ya Aprili, mwaka huu kwa ajili ya kutathmini mwenendo wa uchumi na kuamua Riba ya Benki Kuu itakayotumika katika robo ya pili ya mwaka (Aprili-Juni), mwaka huu.