Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limerudisha kwa jamii kwa kutembelea wagonjwa waliopo katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam tarehe 04 Januari, 2025 ikiwa ni sehemu ya shukurani kwa jamii ambayo ni utaratibu wa Shirika kuwapa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Costa Rubagumya alieleza kuwa Shirika limeamua kurudisha kwa jamii ikiwa ni sehemu ya shukurani kwa mafanikio ya Shirika ambapo mwaka 2024 limeweza kutoa huduma bora pamoja na mahitaji ya umeme kuongezeka lakini liliweza kuongeza uzalishaji kwa kuanza kutumia umeme wa Bwawa la Julius Nyerere na kuhudumia wateja bila kuwa na mgao wa umeme.
“Tumetembelea wagonjwa katika taasisi hii ikiwa ni sehemu ya shukurani ya Uongozi wa TANESCO pamoja na Wafanyakazi wake kutokana na mafanikio yaliyopatikana na tuna mioyo ya furaha kwa kutoa sadaka hii kwa wahitaji hawa,” ameeleza Mhandisi Rubagumya.
Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Michael alishukuru TANESCO kwa kuwezesha msaada huo kwa wagonjwa na kuwa imekuwa ni sehemu ya faraja na furaha katika safari yao ya matibabu.
“Kwa namna ya kipekee napenda kutoa shukurani kwa Uongozi wa TANESCO kwa kuweza kuwakumbuka wagonjwa na kuwapa sadaka ya matendo ya hiari. Sadaka hizo zimekuwa msaada, faraja na furaha katika safari yao ya matibabu”, ameeleza Michael.
Ziara hiyo imetoa faraja kwa wagonjwa na kuimarisha uhusiano kati ya Shirika na Jamii. Matendo haya yanaonesha dhamira ya TANESCO ya kuendelea kusaidia wale wenye uhitaji.