Dar es Salaam
MAABARA ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetunukiwa cheti cha Ithibati cha ubora wa kimataifa cha utoaji huduma za maabara.
Cheti hicho (ISO 15189:2012) kimetolewa Oktoba 2024 na shirika la viwango vya ubora wa maabara kwa nchi za kusini mwa Afrika (SADCAS)
Mapema leo Jumatatu Desemba 30, 2024 akiongea na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa cheti hicho Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi. Dk. Mpoki Ulisubisya ameelezea umuhimu wa ubora wa vipimo kwa wagonjwa na nchi kwa ujumla.
Dk. Mpoki amesema kuwa baaada ya kupata cheti hicho cha ithibati, taasisi ya MOI inafungua milango ya utalii tiba na kuimarisha ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa na nchi mbalimbali duniani.
“Kwahiyo tiba utalii sasa utakuwa na nguvu zaidi, kwa sababu mtu (mgonjwa) anayekuja katika taasisi hii (MOI) atakuwa anatambua kwamba vipimo vinavyofanyika hapa na majibu yake yatakuwa sawasawa na vipimo vya mahali pengine duniani, akiambiwa anaumwa ugonjwa fulani atakuwa na uhakika ugonjwa ule ndio unaomsumbua.
lakini majibu yenye uhakika sio tu yatamsaidia daktari kujua ugonjwa unaomsumbua mgonjwa hata dawa zitakazotolewa zitakwenda moja kwa moja kwenye shida inayomsumbua mgonjwa” amesema mkurugenzi mtendaji huyo kuongeza kuwa
“Katika nchi yetu serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa sana upande wa vifaa tiba pia rasilimali watu, lengo ni kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaotoka hapa nchini na nchi mbalimbali”
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maabara wa MOI, Nsiande Ndosi amesema kuwa mchakato wa kupata cheti hicho cha ithibati ulianza mwaka 2021 ambapo ameishukuru Wizara ya Afya na Shirika lisilo la Kiserikali linahohusika na masuala ya afya MDH, kwa mchango na msaada wao mkubwa katika kufanikisha jambo hilo.
“Tulianza mchakato mwaka 2021 kwa jitihada kubwa kuhakikisha tunafikia malengo ya kimataifa ya kuwa na ithibati kama miongozo ya wizara (wizara ya afya) inavyodai,” amesema Nsiande.