Home KITAIFA RUANGWA KWA MAENDELEO, IMEWEZEKANA-MAJALIWA

RUANGWA KWA MAENDELEO, IMEWEZEKANA-MAJALIWA

*Asema Rais Dk. Samia anamchango mkubwa kwenye Maendeleo ya Wilaya hiyo.

Lindi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Wilaya ya Ruangwa imepiga kasi kubwa ya maendeleo ambayo imewawezesha wakazi wa Wilaya hiyo kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Desemba 29, 2024 wakati alipozungumza na mamia ya Wakazi wa kijiji ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema kuwa Wilaya hiyo changa ilikuwa na changamoto nyingi kwenye Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu ikiwemo barabara, maji, Umeme, Uwekezaji na hata kwenye michezo “Changamoto hizi zilitufanya tuje na kaulimbiu ya “Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana, na sasa imewezekana”

Amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wilaya hiyo kutokana na fedha ambazo amekuwa akitoa zilizowezesha kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati.

Akizungumza kuhusu Sekta ya ElimuMajaliwa amesema kuwa Wilaya ya Ruangwa ilikuwa na vijiji vichache kati ya tisini vilivyokuwa na shule za msingi lakini hivi sasa kila kijiji kina shule ya msingi “Na tunaendelea kujenga kwenye vitongoji”

“Kwa upande wa shule za sekondari tumemaliza kata zote kujenga shule za Sekondari kwenye Wilaya hii na tunachokifanya sasa ni kuongeza shule kwenye kata zenye msongamano mkubwa na hapa Mbekenyera tulikuwa na shule ya Tarafa, lakini baada ya kuona kuna msongamano wa wanafunzi, tumejenga shule nyingine pale Mkutingombe,”amesema.

Aidha, amesema kuwa Sekta ya Afya katika wilaya hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo inauwezo wa kutoa hadi huduma za kibingwa.

Ameongeza kuwa Wilaya hiyo imefanikiwa kujenga mtandao wa barabara za lami katika maeneo mbalimbali na mpango wa kuendelea kujenga barabara za lami unaendelea “Itakuja barabara ya kutoka Masasi kwenda Kiranjeranje, na sasa Masasi kwenda Nachingwea mkandarasi yupo, Ruangwa kwenda Nachingwea Mkandarasi yupo na ameanza kazi na tunajenga kilomita 21 kutoka Ruangwa mjini mpaka Namichiga kwa kiwango cha lami”

Majaliwa alizungumzia sekta za, kilimo, maji na uwekezaji na kusema kuwa kazi kubwa imefanyika na Serikali inaendelea kuziwekea mikakati endelevu sekta hizo.

“Kwenye sekta ya nishati, tumeshapeleka umeme kwenye vijiji vyote na sasa tunaenda kwenye mradi wa vitongoji, ndugu zangu wananchi, tumeshapeleka laini, ni wakati wenu sasa kuvuta umeme,”amesema.

Awali, Majaliwa alitembelea kiwanda cha kubangu korosho cha Naunambe Cashewnuts kinachomilikiwa na Muwekezaji Mzawa Bw. Juma Chambone na kina thamani ya Shilingi milioni 250. Kiwanda hicho kipo katika kijiji cha Mbekenyera

Pia aligawa vifaa vya muziki vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa bendi ya Mkurupuko Jazz bendi iliyopo kwenye kijiji cha Mbekenyera.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here