Home KITAIFA WATENDAJI WA HALMASHAURI WAPIGWA MSASA MATOKEO YA SENSA YA MWAKA 2022

WATENDAJI WA HALMASHAURI WAPIGWA MSASA MATOKEO YA SENSA YA MWAKA 2022

Na Josephine Majura na Chedaiwe Msuya , Mbeya

NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema kuwa matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 yanalenga kuisaidia Serikali na wadau wengine kufuatilia na kufanya tathmini juu ya utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo katika Sekta zote nchini.

Hayo yameelezwa Disemba, 21 2024kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usambazaji na Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, yaliyotolewa kwa Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbalizi mkoani Mbeya.

“Matokeo hayo ndio yatakuwa dira yetu katika kufanya maamuzi yote ya msingi yanayohusu uanzishaji wa miradi mipya, uimarishaji na kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi zikiwemo za kijamii kama elimu, afya, maji na huduma nyingine kama za kiuchumi na miundombinu,” amesema Mwanaidi.

Aidha, amesisitiza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watendaji na viongozi mbalimbali kutumia matokeo ya sensa na takwimu mbalimbali wanapozungumza na wananchi ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa takwimu katika maendeleo.

Naibu Waziri Mwanaidi, amewataka pia washiriki wa mafunzo hayo kufikisha elimu kwa wananchi kupitia vikao vinavyowakutanisha viongozi, wataalamu na wananchi na wadau wa maendeleo ili kujenga uelewa wa kuyafahamu masuala hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mifumo ya Taarifa za Kijiografia kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Benedict Mugumbi kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, amesema kuwa ofisi hiyo ipo tayari kutoa mafunzo hayo katika mikoa mbalimbali  ili  kuhakikisha mafunzo hayo yanafika kwa wananchi wote.

Mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi yamefanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini.

Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambaye ni  Mbunge wa Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njeza aliishukuru Serikali kwa kuendelea kupeleka fedha ambazo zinasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.

Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia mbalimbali kwa wananchi jimboni humo ambao walipisha maeneo yao kwa Serikali ili yaweze kutumiwa na Serikali kwa ajili ya kuyaendeleza kupitia miradi mbalimbali ikiwemo upanuaji wa barabara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here